Ajibu Aendelea Kung’alisha Nyota Yake Msimbazi

ajibu

Ikiwa ni tunzo ya 4 tangu kuanza kwa zoezi la kumchagua mchezaji bora wa mwezi ambapo zoezi hili lilianzishwa mwezi Septemba, 2015 likiwa na dhumuni la kuongeza morali na kuwazawadia wachezaji wanaofanya vizuri.

Mshambuliaji Ibrahim Ajibu ameshinda kwa mara ya pili tuzo ya mchezaji bora mwezi Januari, 2016 baada ya kupigiwa kura kwa wingi na wanachama, mashabiki na wapenzi wa Simba na soka la Tanzania kwa ujumla kupitia simu za mkononi ambao pia wamejiunga na huduma ya Simba News pamoja na kwenye mitandao rasmi ya kijamii ya Simba Facebook www.facebook.com/simbatanzania Twitter na Instagram @simbasctanzania.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam Rais wa Simba Evans Aveva amesema, “sisi kama uongozi wa klabu yetu ya Simba tunaamini katika kuwapa motisha wachezaji wetu kila iitwapo leo na hii ni katika kuongeza chachu ya maendeleo si tu kwa mchezaji bali kwa klabu nzima kwa ujumla, Ajib anashinda tunzo hii kwa mara ya pili mfululizo.

Wote mtakubaliana nami kuwa kwa kiwango anachoonesha mshambuliaji Ajib ni kweli mshabiki, wanachama na wapenzi wa Simba hawajakosea kumchagua tena mchezaji huyu”

Napenda kutoa wito kwa wachezaji wetu wote kuendelea kujituma zaidi kwani mashabiki wao wakiongozwa na uongozi mzima tunamatumaini makubwa msimu huu 2015/2016, tukiamini kwenye falsafa yetu ya SIMBA NGUVU MOJA, aliongeza Rais Evans Aveva.

Mkurugenzi Mkuu wa EAG Group ambao ni washauri na watekelezaji wa Masoko na Biashara wa Simba, Imani Kajula amesema, “EAG Group inapenda kusisitiza kuendelea kuongeza utayari wake katika kushirikiana na klabu ya Simba kwenye kutoa motisha kwa wachezaji wa Simba ambapo italeta chachu ya kufanya vizuri zaidi na hivyo kuweza kutengeneza mfumo mzuri wa kuongeza vyanzo vya mapato na hatimaye faida kubwa kwa wachezaji na timu kwa ujumla”.

Simba News ni huduma iliyoanzishwa na Simba ili kuwapa wapenzi wa Simba habari mbalimbali za Simba popote pale walipo ikiwemo matokeo, majina ya wachezaji wanaocheza mechi, usajili na habari nyingine za klabu ya Simba. Kujiunga na Simba News tuma neno Simba kwenda namba 15460 kisha utaletewa ujumbe jibu kwa kutuma neno “OK” na hapo utakuwa umejiunga rasmi, Huduma hii ni maalum kwa Tigo na Vodacom.
Imetolewa na simbasports.co.tz