MSIBA mwingine mzito umelikumba taifa baada ya watu 38 kupoteza maisha katika matukio mawili tofauti, likiwamo la ajali ya basi dogo aina ya Toyota Hiace iliyoua watu 19 wakati ikifanya safari ya wizi mkoani Mbeya.
Tukio jingine limetokea mkoani Shinyanga ambako wachimbaji wadogo 19 wa dhahabu waliokuwa katika mgodi mdogo wa Kalole, wilayani Kahama wamekufa baada ya kufunikwa na kifusi usiku wa kuamkia jana kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha. Matukio hayo ni mwendelezo wa majanga ya ajali ambazo zimekuwa zikitokea kwa takriban wiki mbili mfululizo na kuua mamia ya watu. Zaidi ya watu 980 wamefariki dunia katika ajali za barabara katika muda wa zaidi ya miezi mitatu.
Katika ajali ya basi iliyotokea saa 3:00 asubuhi jana katika Barabara ya Mbeya-Kyela eneo la Kiwira ambalo ni maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege kutokana na magari mengi yanayopata ajali kuonekana kama ndege inayoelekea kutua wakati yakitumbukia kwenye bonde ambalo Mto Kiwira unapita, watu 18 walifariki papo hapo na mwingine mmoja alifariki dunia akiwa Hospitali ya Igogwe.
Dereva wa basi hilo, lililokuwa likipeleka wafanyabiashara kwenye gulio la Kiwira wilayani Rungwe, alikuwa ameamua kufanya safari hiyo badala ya ruti zake za kawaida za kuzunguka mjini Mbeya, baada ya madereva wa mabasi aina ya Toyota Coaster kuwa na mgomo wa kupinga wenzao kupigwa faini kubwa.
Akizungumzia ajali hiyo jana, Mkuu wa Wilaya ya Rungwe, Zainab Mbiro alisema chanzo chake ni mwendo wa kasi katika eneo lenye mteremko ambao una kona kali iliyo takriban kilomita nne kabla ya kuingia Kiwira. Eneo hilo linajulikana kwa ajali nyingi ambazo zimekuwa zinachukua maisha ya watu wengi kila mwaka.
“Basi dogo limetumbukia kwenye Mto Kiwira baada ya dereva kushindwa kukata kona kutokana na kuwa kwenye mwendo kasi katika eneo la mtelemko mkali maarufu kwa jina la Uwanja wa Ndege,’’ alisema.
Eneo hilo la urefu wa kilometa nane za barabara ya kuanzia Uyole kwenda Rungwe, limewekewa vibao vya alama za tahadhari kwa madereva kuwatahadharisha kuwapo kwa miteremko na kona kali.
Kamanda wa polisi wa Mkoa wa Mbeya, Hemed Msangi, akiwa eneo la tukio jana, alisema ajali hiyo iliua watu 18 palepale na mmoja alifariki dunia akipatiwa matibabu kwenye Hospitali ya Igogwe, Kiwira na kwamba watatu walijeruhiwa na wamelazwa hospitalini hapo. Msangi alisema maiti 18 zilipelekwa Hospitali ya Makandana wilayani Rungwe na mmoja alibaki Igogwe. Hata hivyo alishindwa kutaja majina akisema karibu wote hawana vitambulisho.
“Kibaya zaidi ni kwamba gari lililopata ajali ni daladala linalosafiri kati ya Igawilo na Majengo na wafanyakazi wake waliamua kuwachukua wafanyabiashara waliokuwa wakienda kwenye gulio la Kiwira wilayani Rungwe baada ya (Toyota) Coaster kugoma,” alisema.
Mabasi hayo aina ya Toyota Coaster ndiyo yanayofanya safari kati ya mji wa Uyole na Tukuyu. Ajali hiyo inafanya idadi ya waliokufa kati ya Januari Mosi na Aprili 12 mwaka huu kufikia 988, kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Kamanda Mpinga hivi karibuni.
Kamanda Mpinga alisema watu 866 walikufa na wengine 2,363 kujeruhiwa kati ya Januari na Machi, wakati wengine 103 wamepoteza maisha na 138 kujeruhiwa kati ya Machi 11 na Aprili 12 mwaka huu.
Kuhusu mgomo wa mabasi aina ya Toyota Coaster, Kamanda Msangi alisema chanzo ni madereva kupinga faini ya Sh250,000 iliyotolewa na maofisa wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchikavu (Sumatra) kwa madereva wawili baada ya kukiuka taratibu za usafirishaji.
Tukio la kugoma kwa madereva hao ni la pili kwa wiki hii, la kwanza likiwa limetokea Jumatatu ambalo lilisuluhishwa baada ya viongozi wa Sumatra kukutana na wadau hao pamoja na polisi na kuafikiana kwamba mabasi yaliyokamatwa yaachiwe. Mwenyekiti wa madereva hao, Damdam Mwandubya hakuweza kupatikana, lakini dereva aliyejitambulisha kwa jina la Geofrey Masanja alisema waligoma ili kushinikiza mabasi yaliyopigwa faini, yaachiwe.
Maafa Shinyanga
Mkoani Shinyanga wachimbaji wadogo 19 walifukiwa na kifusi wakiwa ndani ya mgodi mdogo wa Kalole kutokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha. Wachimbaji hao walikuwa wameingia kwenye mashimo nane ambayo baadaye yalibomoka kutokana na kufunikwa na udongo, jambo lililosababisha vifo vyao.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya alisema vijana hao waliingia katika mashimo hayo saa 12:00 jioni kwa lengo la kuiba mawe baada ya muda wa kufanya kazi kumalizika.
“Unajua hawa ndugu zetu ni wale wachimbaji wasiokuwa na mashimo ambao muda ukiisha wa kazi huingia kwenye mashimo hayo bila kuangalia usalama na ndivyo ilivyotokea kwa wachimbaji hao,” alisema Mpesya.
Mpesya alisema kazi ya kufukua maiti hizo lilianza, lakini lilikwama kutokana na hali ya unyevunyevu kwenye mashimo hayo ambayo bado yanaendelea kutitia.
“Kati ya maiti 19, saba tayari zimeshatambuliwa na ndugu zao huku nyingine mbili zikiwa bado hazijatambuliwa na tayari tumeomba mashine ya kufukua na ya kunyonya maji kutoka mgodi wa Bulyanhulu ili itusaidie,” alisema
Hata hivyo, Mpesya alisema idadi hiyo inaweza kuongezeka baada ya kazi ya kufukua kukamilika kwa kuwa hawawezi kujua kama maiti hizo 19 ndio idadi pekee ya watu waliokuwemo ndani ya mashimo hayo.
“Tunasubiri wenzetu kutoka mgodi wa Bulyanhulu waje waone kwanza mitambo ipi ambayo inaweza kutumika kuyafukua mashimo hayo kwa kuwa ufukuaji wa kienyeji tuliokuwa tukitumia tumeusimamisha kutokana na mashimo hayo kuendelea kutitia,” alisema Mpesya.
Machimbo hayo yaliyoko katika kijiji cha Kalole katika kata ya Lunguya Halmashauri ya Msalala, ni moja kati ya migodi ya wachimbaji wadogo wanaokisiwa kufikia 30,000 na tayari wengi wao wamejipatia mamilioni ya pesa kwa uchimbaji huo wa kienyeji hali ambao si salama.
CHANZO: http://www.mwananchi.co.tz