Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed shein amesema jumla ya watu 106 hadi sasa wamethibitika kupoteza maisha baada ya Meli ya abiria na mizigo ya Mv. Spice Islander usiku wa kuamkia Septemba 10, 2011.
Wakati Dk. Shein akitoa taarifa hiyo, Rais wa Tanzania, Jakaya Kiwete alipowatembelea majerui jana jioni, ameelezwa kuwa watu 192 wamethibitika kupoteza maisha na miili yao kuopolewa, huku wengine 630 wakiwa wameokolewa kwenye ajali hiyo ya meli. Hadi sasa haijulikani ilikuwa imebeba abiria wangapi.
Mv. Spice Islander ilizama ikiwa safarini ikitokea Unguja kwenda Pemba. Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Rais Dk. Shein, amesema watu 597 wameokolewa wakiwa hai na wamepelekwa Hospitali ya Kivunge na wengine Hospitali ya Mnazi Mmoja. Katika taarifa hiyo amesema baadhi yao wameruhusiwa kurudi majumbani mwao.
Hata hivyo amesema Serikali itaendelea kuwahudumia waliokuwa hospitali kwa shida zao zote hususan chakula na mahitaji mengine ya msingi. Amesema kutokana na maafa hayo Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetangaza siku tatu za maombolezo kuanzia leo Septemba 11, 2011. Aidha, katika kipindi hicho sherehe na tafrija zote hazina budi kusitishwa. Kadhalika bendera zitapepea nusu mlingoti.
“Kwa niaba ya Serikali, nachukuwa nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa watu wote walioguswa na msiba wetu huu mzito. Pamoja na hayo natoa rambi rambi kwa wafiwa wote. Pia, nawatakia rehma na maghfira waliotangulia mbele ya haki na walionusurika nawaombea shufaa wapone haraka na Mwenyezi Mungu awasahaulishe kumbukumbu zote mbaya za tukio hili ili wapate kuendelea na maisha yao katika hali ya kawaida,” alisema Dk. Shein katika taarifa hiyo. Alitaja ajali hiyo kuwa ni msiba mkubwa sana kwa Zanzibar na Taifa kwa jumla.
Akielezea jitihada za Serikali tangu ilipopata taarifa, amesema; “Baada ya kupata taarifa hii, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilichukuwa hatua za haraka za kulishughulikia tukio hili. Viongozi wa Kitaifa na wengineo wamekuwa katika harakati za kushughulikia jambo hili tangu alfajiri ya leo milango ya saa 9.00 alfajiri.”
Amesema katika kuokoa, Serikali imetumia vyombo vya Ulinzi na Usalama vilivyopo katika harakati za uokozi na kuwahudumia walioathirika na janga hili. Aidha, Serikali ilishirikiana na vyombo vya usafiri vya watu binafsi na taasisi mbali mbali za huduma.
“Ni dhahiri kuwa katika tukio kama hili watu hupatwa na fadhaa na mshtuko lakini tukiwa waumini hatuna budi kuamini kuwa huu ni mtihani wa Mwenyezi Mungu Subhanahu Wataala. Ni wajibu wetu tuupokee mtihani huu na tushukuru. Mwenyezi Mungu anatutaka tuwe na subira katika kukabiliana na mitihani kama hii. Dini yetu inatufunza kuwa hapa duniani Mola atatupa mitihani mbali mbali ili kutupima imani zetu na bila shaka huu ni mmoja wapo. Mwenyezi Mungu anawapenda wenye kushikamana na imani na subira.” amesema Dk. shein.
Pamoja na hayo ametoa wito kwa wananchi kuwa wastahamilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba na maafa, na kuongeza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inashughulika kikamilifu ikiwa ni pamoja na kusaidia kuwatambua waliofariki, kuwasaidia waliookolewa na waliopata maumivu katika janga hili.
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itashughulikia maziko kwa wale wote waliofariki. Kwa wale watakaotambuliwa, jamaa zao wataruhusiwa kuwachukua maiti hao kwa ajili ya mazishi na kwa wale waliokuwa hawakutambuliwa kwa vile wamefariki kwa maji ya chumvi wote watazikwa hapa Unguja katika eneo moja huko Kama lakini kila mmoja atazikwa katika kaburi lake. Mipango ya mazishi itatangazwa rasmi na Kamati ya Maafa ya Zanzibar kwa kushirikiana na Kamati ya Zanzibar ya Mazishi .
Serikali itaandaa hitma maalum ya marehemu wote ambayo pia itahudhuriwa na baadhi ya viongozi wakuu. Aidha, Rais na viongozi wetu watapangiwa ratiba ya kwenda kwenye maeneo mbali mbali Unguja na Pemba kwa kuwapa pole wafiwa. Vile vile majina ya waliohai yatatangazwa kwa utaratibu maalum utatangazwa na Kamati ya Maafa. Ni vyema wananchi wakafuatilia habari sahihi za tukio hili kupitia vyombo vya habari ili kuepuka kupata taarifa zisizoaminika. Juhudi za uokozi zinaendelea na wananchi mtaendelea kuarifiwa ipasavyo.
Aidha, alizishukuru taasisi za huduma mbali mbali wakiwemo wafanyabiashara, mabalozi, Wabunge, Wawakilishi na wale wote walizojitokeza kutoa misaada. Shukurani maalum ziwaendee wananchi wa Nungwi kwa ushirikiano mkubwa walioutoa katika uokozi pamoja na vyombo vya habari kwa kutoa taarifa kwa wananchi.
Aliongeza kuwa kwa upande wa Serikali, itaendelea kuhakikisha wenye vyombo vya usafiri baharini wanatekeleza wajibu wao hasa kuhusu usalama ipasavyo. Uchunguzi utafanywa kutambua kikamilifu sababu ya ajali hii na taarifa rasmi itatolewa kwa wananchi. “Serikali ipo pamoja na wananchi wote katika maafa haya. Inna Lilah Wainna Ilayhi Rajiun!,” amesema Dk. Shein.