Na Mwandishi Wetu
Geita
WATU 15 wakiwemo watoto wawili, askari polisi mmoja wa
jijini Mwanza wamepoteza maisha na wengine 67 kujeruhiwa
vibaya katika ajali iliyohusisha basi la kampuni ya
Sheraton lenye namba T 268 AJC na basi la Bunda Expres
namba T 810 BDW baada ya kugongana uso kwa uso eneo la
Kijiji cha Chibingo Wilaya ya Geita mkoani Mwanza.
Ajari hiyo ambayo imetokea jana mjini hapa majira ya saa
tatu asubuhi eneo la barabara kuu ya Mwanza-Bukoba
imehusisha mabasi mawili pamoja na roli la mizigo aina
ya Fusso lenye namba za usajili T 823 BDV baada ya basi
la Sheraton lililokuwa likitoka Ushirombo Shinyanga
kwenda Mwanza, kutaka kulipita lori lililokuwa likipanda
kilima cha Chibingo.
Taarifa zinaeleza kuwa kabla ya kulipita gari hilo
lilikutana uso kwa uso na basi la Bunda lililokuwa
likitoka mkoani Mwanza kuelekea Karagwe Mkoa wa Kagera
na ndipo ajali hiyo ilipotokea.
Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo wamesema ajali hiyo
imesababishwa na mwendo kasi wa madereva wa mabasi hayo
huku yule wa basi la Sheraton akitupiwa lawama kwa
kushindwa kufuata sheria za barabarani kutokana na
kutaka kulipita gali lililokuwa kwenye kilima bila
kuhofia atari yoyote eneo hilo.
“Tulikuwa tukitokea Shinyanga kwenda Mwanza na basi la
Sheraton tulipofika Kijiji cha Chibingo dereva wetu
alijalibu kulipita gari la mizigo, lakini alishindwa
kulimudu gari kisha kugongana uso kwa uso na basi la
Bunda hali iliyosababisha vifo…huu ni ukiukaji wa
sheria za barabarani,” alisema, Yunusu Mathias.
Mmmoja wa majeruhi, Johnas Kalokola ambaye ni mwanafunzi
wa Sekondari ya Ihungo Bukoba, alisema dereva wa Bunda
alijitahidi kulikwepa basi la Sheraton kwa kunusuru
maisha ya abiria waliokuwa wakisafiri kuelekea Karagwe,
lakini kutokana na mwendo kasi wa mabasi hayo
yaligongana na baadhi ya abilia kupoteza maisha, viungo
vya mwili na mali zao.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Wilaya ya Geita, Dk.
Abdallah Dihenga amethibitisha kupokea miili 15 na
majeruhi zaidi ya 60 na kuongeza kati yao watu sita
wamepelekwa katika hospital ya rufaa ya Bugando Mwanza
baada ya hali zao kuwa mbaya.
Alisema madaktari wanaendelea kuwahudumia majeruhi hao
na hali zao zinaendelea vizuri baada ya wengine saba
kutibiwa na kuruhusiwa, huku akiwataka ndugu, jamaa na
marafiki kufika hospitalini hapo kwa ajili ya kutambua
miili ya marehemu ambao wamehifadhiwa chumba cha maiti
hospitalini hapo.
Kutokana na ajali hiyo mamia ya wananchi wamefulika
katika eneo la tukio wakisaidia kutoa miili ya marehemu
na majeruhi katika magari yaliyo gongana uso kwa uso
licha ya zoezi hilo kuwa gumu kutokana na ukosefu wa
vifaa vya kutoklea huduma ya kwanza .
Mkuu wa Wilaya ya Geita, Philemon shelutete na Mbunge wa
Jimbo la Busanda, Lolensia Bukwimba ambao wamefika eneo
la tukio na kueleza kusikitishwa na ajali hiyo na
kutamka ni janga la kitaifa, hivyo kuwataka Watanzania
kuomboleza juu ya vifo v ya wananchi hao.
Hata hivyo Shelutete amewataka wamiliki wa magari ya
abiria kuajiri madereva wenye ujuzi wa kutosha kwa lengo
la kupunguza ajali na kudai iwapo madereva hao
wangezingatia sheria za usalama ajali hiyo isinge tokea.