Ajali nyingine yaua wanane Rukwa

Na Mwandishi Wetu
Sumbawanga

WATU wanane wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa vibaya baada ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda kusherehekea Sikukuu ya Pasaka kuacha njia na kupinduka.

Ajali hiyo imetokea usiku wa kuamkia mkesha wa Pasaka kwenye Milima ya Lyamba Lyamfipa ulipo mpakani mwa wilaya za Mpanda na Nkasi mkoani Rukwa.

Kwa mujibu taarifa zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage, ajali hiyo ambayo ilitokea majira ya saa nane usiku, ilihusisha gari aina ya Fuso mali ya Basilio Mbwilo, ambaye Diwani wa Kata ya Kirando Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, kati ya waliokufa, yumo dereva wa gari hilo ambaye jina lake halikuweza kutambuliwa mara moja, hata hivyo maiti hiyo na nyingine nne zimesafirishwa kwenda mjini Sumbawanga kwa utambuzi.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Mpanda, Dk. Emanuel Kamgobe, aliwataja marehumu hao kuwa ni Kasipisti Guni mkazi wa Urambo- Tabora na Freddy Kisesa (29) mkazi wa mjini Mpanda.

Dk Kamgobe alisema maiti nyingine hazijatambuliwa na zimepelekwa mjini Sumbawanga ili ziweze kutambuliwa huku majeruhi, wawili wote wanawake hali zao ni mbaya wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda mmoja ametambuliwa kuwa Elizabeth Philipo (20), mkazi wa Urambo mkoani Tabora ambapo mwingine bado hajatambuliwa.

Majeruhi wengine ambao wamelazwa hospitalini hapo wametambuliwa kuwa ni Jofrey Isenga – (25), mkazi kijiji cha Matai, Samson Bunenge (50 mkazi wa kijiji cha Mwankulu, Rashid Idd (43) mkazi wa mjini Mpanda na Lusekelo Kipemba (32) mkazi wa mjini Sumbawanga.

Dk. Kamgobe aliongeza kuwa majeruhi mwingine ambaye ni Dk. Bernad Mbushi (55) anayefanya kazi hospitalini hapo alitipiwa na kuruhusiwa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Isuto Mantege lori hilo aina ya FUSO lenye namba T158 BDZ lililokuwa likitoka mjini Sumbawanga lilipinduka wakati likiteremka miteremko mikali ya Lyamba.

Alisema pamoja na abiria lori hilo likuwa lisheheni vifaa vya ujenzi ikiwemo mifuko ya saruji na chokaa pia lilikuwa limebeba watu waliokuwa wakitokea mjini Sumbawanga kwenda mjini Mpanda kushehekea Sikukuu ya Pasaka.

Alisema chanzo cha ajali hiyo ni uzembe na kwamba waliokufa ni nane wanaume wakiwa watano na wanawake wawili.

Alisema maiti sita ambazo hazijatambuliwa zimesafirishwa mjini Sumbawanga ambapo mbili zimehifadhiwa hospitali ya wilaya mjini Mpanda zimekwisha tambuliwa.