Na Joyce Anael, Moshi
WATU 11 wamefariki dunia na wengine 24 kujeruhiwa vibaya katika ajali mbaya iliyotokea katika eneo la barabara ya kibosho nje kidogo ya mji wa moshi baada ya gari la mizigo aina ya fuso kugongana uso kwa uso na gari la abiria iliyokuwa imebebeba wafanyakazi wa kampuni ya kahawa ya Kilimanjaro Platation.
Ajali hiyo ambayo ilitokea julai 28 majira ya saa moja na nusu usiku ilihusisha gari la Lim Safari lenye namba za usajili T 489 BJR Mitsubishi Fuso lililokuwa limebeba wafanyakazi wa kampuni ya kahawa waliokuwa wametoka kuchuma kahawa Kibosho kuelekea Machame likiendeshwa na Judika Uromi (30-35)mkazi wa machame wilayani Hai pamoja na gari T 884 BFL Mitsubishi Fuso Lori lililokuwa limebeba nyanya likiendeshwa na Faeli Kaaya(52) mkazi wa Leguruki wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Akizungumzia ajali hiyo, Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai mkoani Kilimanjaro, Obadia Nselu alisema kati ya watu 11 waliofariki dunia tisa ni wanaume huku wanawake wakiwa wawili ambapo waliojeruhiwa wanaume ni 15 na wanawake Tisa.
Alisema marehemu waliotambuliwa ni madereva wawili ambao ni Judica Ndeonasia dereva wa gari la Lim Safari na Faeli Kaaya dereva wa gari la mizigo. Aidha alisema majeruhi Saba kati ya majeruhi 24 wamelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika hospitali ya Rufaa ya KCMC ambao ni Ashura Abdallah, Michael Ismail wote wanakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 -30, Stephano Mushi (71)na wanaume wanne ambao bado hawajatambuliwa majina yao.
Aliwataja Majeruhi wengine kuwa ni Ethibend Mbowe(56), Raymond Emanuel(29), Evalin Uroni(9), Peter Samson(20), Grace Ulomi (43), Mwamvita Ulomi(30), Mushi Rose(26), Estomih Amos( 30), Goodluck Estory(30), Christopher Idd(29), Abimael Massawe(29), Barick Ramadhan(30), Joyce Lyamuya(31) na mtu mwingine aliyefahamika kwa jina moja la Peter( 56) pamoja na wanaume watatu ambao bado hayajafahamika.
Kwa mujibu wa Nselu ajali hiyo imehusisha magari manne ambayo ni gari la abiria la Lim Safari, Gari la mizigo, gari lenye Namba za usajili T 327 BET aina ya Toyota Landcruiser Prado pamoja na gari la abiria la Fresh Coach lenye namba T 673 BCD Scania ambayo yalikwaruzwa kwa pembeni na gari la Lim safari kabla ya kugongana uso kwa uso na Lori lililokuwa limebeba nyanya.
Nselu alieleza kuwa gari la Lim Safari lililokuwa likitokea Kibosho kuelekea Machame lilipofika Barabara ya Kibosho eneo la kata ya Karanga Manispaa ya Moshi lilihama upande wake na kwenda upande mwingine wa kulia ambapo lilikuta gari aina ya Landcruiser Prado pamoja na gari la Fresh Coach yaliyokuwa yameegeshwa pembeni ya barabara baada ya kuona gari Hilo la Lim Safari likija kwa mwendo kasi hali ambayo ilisababisha ligongane uso kwa uso na Lori la mizigo.
Alisema uchunguzi wa awali uliofanywa na jeshi la polisi umebaini kluwa chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa gari la abiria la Lim Safari kupita gari lingine bila kuchukua tahadhari katika eneo ambalo ni la mteremko mkali.
Wakielezea tukio hilo baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo wamelalamikia madereva kuendesha magari kwa mwendo kasi pamoja na askari polisi kufika eneo la tukio na kushindwa kuokoa majeruhi waliokuwa wamenasa katika magari hayo mawili kutokana na kukosa vifaa hali ambayo iliwalazimu wananchi wa eneo hilo kutumia mashoka kukata vyuma vya magari ili kuokoa maisha ya abiria hao na kuondoa maiti zilizokuwa zimenasa kwenye magari hayo.
Nao baadhi ya wakazi wa eneo hilo walisema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakilalaimikia kuwekewa matuta katika eneo hilo bila mafanikio hali ambayo imekuwa ikisababisha kutokea kwa ajali nyingi hasa zinazohusisha wanafunzi wakati wakivuka barabara.
Walisema endapo serikali haitachukua hatua za makusudi ikiwa ni pamoja na kujenga matuta katika eneo hilo watajichukulia hatua za kufunga barabara hiyo kwa kuwa idadi ya watu wanaopoteza maisha katika eneo hilo ni kubwa.
Miili ya marehemu imehifadhiwa katika hospitali ya rufaa ya KCMC na majeruhi wote 24 wamelazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya matibabu.