Airtel Raising Stars Wasichana Kupongezwa, Twiga Stars Kucheza na Zambia

Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

TIMU ya mpira wa miguu ya wasichana ya Airtel Raising Stars (ARS) ya Tanzania imeandaliwa hafla ya kuipongeza kwa kunyakua ubingwa katika mashindano ya Afrika yaliyofanyika nchini Nigeria. Hafla hiyo ya kuipongeza pamoja na kupata chakula cha mchana itafanyika Septemba 24 mwaka huu saa 6 mchana kwenye hoteli ya Kilimanjaro Kempinski na kuongozwa na Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara.
 
Timu hiyo iliyorejea nchini Septemba 23 mwaka huu usiku katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo iliifunga Kenya. Kwa upande wa wavulana, timu hiyo ilitolewa na Zambia katika hatua ya nusu fainali.
 
Michuano hiyo ilishirikisha timu kutoka nchi za Burkina Faso, Chad, Congo Brazzaville, Gabon, Ghana, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Kenya, Madagascar, Malawi, Niger, Nigeria, Tanzania, Uganda na Zambia.
 
Kombaini ya timu hizo zilizokuwa chini ya makocha Rogasian Kaijage na Abel Mtweve iliundwa baada ya mashindano ya Airtel Raising Stars yaliyohusisha wasichana na wavulana wenye umri wa chini ya miaka 17 na kufanyika jijini Dar es Salaam wiki ya kwanza ya Septemba mwaka huu.
 
TWIGA STARS YAPANGIWA ZAMBIA AWC
Timu ya Taifa ya mpira wa miguu ya wanawake (Twiga Stars) imepangiwa kucheza na Zambia katika mechi za kutafuta tiketi ya kucheza Fainali za Afrika kwa Wanawake (AWC) zitakazofanyika mwakani nchini Namibia.
 
Twiga Stars itaanzia ugenini jijini Lusaka ambapo mechi ya kwanza itachezwa kati ya Februari 13 na 15 mwakani wakati ile ya marudiano itafanyika kati ya Februari 28 na Machi 2 mwakani jijini Dar es Salaam.
 
Iwapo Twiga Stars itafanikiwa kuitoa Zambia, raundi ya pili ambayo ndiyo ya mwisho itacheza na mshindi kati ya Botswana na Zimbabwe. Mechi ya kwanza itakuwa Dar es Salaam kati ya Mei 23 na 25 mwakani wakati ile ya marudiano itakuwa kati ya Juni 6 na 8 mwakani.
 
Nchi 25 zimeingia katika mashindano huku mabingwa watetezi Equatorial Guinea, makamu bingwa Afrika Kusini na Cameroon iliyoshika nafasi ya tatu katika fainali zilizopita zikiingia moja kwa moja katika raundi ya pili.
 
RHINO KUIKARIBISHA ASHANTI ALI HASSAN MWINYI
Rhino Rangers na Ashanti United zinapambana katika mechi pekee ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) itakayochezwa kesho (Septemba 25 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora.
 
Wakati Rhino Rangers ilitoka sare ya bao 1-1 katika mechi yake iliyopita jijini Tanga dhidi ya Mgambo Shooting Stars, Ashanti United inashuka uwanjani huku ikiwa na kumbukumbu mbaya ya kutandikwa mabao 3-0 na Kagera Sugar katika mechi iliyochezwa Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
 
Boniface Wambura Mgoyo, Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)