Watoto wa shule ya awali ya Mbuyuni iliyopo wilayani Kinondoni jijini Dar es Salaam wamenufaika na msaada wa madawati kutoka kwa kampuni ya Matangazo na Mawasiliano ya Aggrey&Clifford yenye thamani ya shilingi milioni 10.Pia kampuni hiyo imetoa vifaa mbalimbali vya kusomea kwa shule hiyo ambayo pia inatoa elimu kwa watoto wenye ulemavu wa akili.
Msaada huo umetolewa kupitia taasisi isiyo ya kiserikali ya Hassan Maajar Trust,nayo ya jijini Dar es Salaam ambayo imekuwa ikijishughulisha na kuboresha mazingira ya watoto kusomea kwa kutoa misaada ya madawati na vifaa vya kusomea mashuleni ikiwemo vitabu na tangu ianzishwe tayari imetoa misaada kwa shule mbalimbali nchini.
Akiongea katika hafla ya kukabidhi msaada huo iliyofanyika katika shule ya msingi Mbuyuni Meneja wa Mawasiliano na matangazo wa Aggrey&Clifford Bw.Oliver Mutere alisema kuwa msaada huo ni kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.
“Kampuni yetu ambayo ina mtamdao katika ukanda wa Afrika Mashariki na ikiwa imeajiri wataalamu wa Nyanja mbalimbali inajua umuhimu wa elimu bora na ndio maana tumetoa msaada huu kuwawezesha watoto hawa wasome katika mazingira mazuri ili waje kuwa wataalamu wazuri katika siku zijazo na tutaendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha elimu nchini”.Alisema.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi Hassan Maajar Trust ZenaTenga, alisema ana imani kuwa msaada huu utawanufaisha wanafunzi wengi katika shule ya Mbuyuni watakaotumia madawati haya “Mazingira bora ya kusomea ni jambo la muhimu katika kuboresha elimu nchini na huwezi kuongelea elimu bora wakati watoto wanasoma wakiwa wamekaa sakafuni”.Alisema na kutoa wito kwa makampuni na taasisi zingine kulivalia njuga tatizo la upungufu wa madawati mashuleni na kulimaliza kabisa.
Kwa upande wake Mwalimu Mkuu wa Shule ya Mbuyuni Dorothy Malecela alishukuru kwa msaada huo ambaye shule yake imepata na alitoa wito kwa wafadhili wengine kuendelea kujitokeza kusaidia jitihada za serikali katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zilizopo katika ufanikishaji wa kutoa elimu bora.