Na Mwandishi wetu
Arusha, Juni 10, 2012 (EANA) – Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) anayeshughulikia Shirikisho la Kisiasa, Dk. Julius Rotich amesema kanda hiyo inahitaji mkakati madhubuti na unaoweza kutekelezeka ili kupambana na changamoto za vitisho vya usalama.
‘’Tunakiwa tujiweke tayari kimkakati kwa kuzingatia vitisho vya kiusalama kama vile kwenye bahari,uharamia,biashara ya fedha,ugaidi na uhalifu wa kwenye mitandao ikiwa ni miongoni mwa vitisho vilivyopo, kwa lengo la kuhakikisha kwamba amani na utulivu vinabaki kuwa vipaumbele katika nchi za Afrika Mashariki,’’ alisema.
Dk. Rotich alisema hayo alipokuwa anafungua mkutano wa siku tano wa watasalamu wa EAC kutathmini mkakati wake wa Amani na Usalama, mjini Dar es Salaam, Tanzania, Alhamisi.
Katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Ofisa wa Amani na Usalama wa EAC, Didacus Kaguta, Naibu Katibu Mkuu huyo alisisitiza kuzingatia na kuendeleza masuala ya amani na utulivu ambayo ni nguzo muhimu katika agenda ya mtangamano wa EAC.
Mkataba wa EAC unatambua amani na usalama kuwa ni masuala muhimu ya awali kabisa kufanikisha mtangamano huo ambao ni muhimu zaidi kwa sasa wakati kanda inaelekea katika majadiliano ya muungano wa fedha.
Muungano wa fedha ni hatua ya tatu ya mtangamano wa EAC ikiwa imetanguliwa na Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja.
Naye Mwenyekiti wa kikao hicho David Njoka alisema kanda hiyo ya EAC haiwezi kukaa kimya bila kushughulikia vitisho vipya vya usalama ambavyo vinaweza kuvuruga lengo la kuwa na Afrika Mashariki iliyoungana na yenye mafanikio.
Mkutano huo uliohudhuriwa na wataalamu kutoka jeshi, polisi, usalama,magereza,mahakama na sekta ya sharia,uliratibiwa na EAC.