Na Ronald Ndungi, EANA-Arusha
BENKI ya Maendeleo Afrika (AfDB) imetoa changamoto kwa nchi wananchama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha ushirikiano wao katika sekta ya nishati. Mkurugenzi wa Kanda wa AfDB, Gabriel Negatu alisema kwamba hatua hiyo itavutia soko kubwa zaidi la wawekezaji katika katika kanda hiyo.
“Kutakuwa na upatikanaji wa fedha zaidi katika kanda iwapo kutokuwepo na miradi ya maana,” Negatu alisema.
Hivi sasa EAC inakabiliwa na tatizo kubwa la ukosefu wa nishati ya kutosha na hivyo kufanya kanda hiyo ya kiuchumi kushinwa kushindana ipasavyo katika sekta mbalimbali za kiuchumi. EAC mara nyingi imekuwa ikifanya vibaya katika utafiti wa dunia unaopima gharama za ufanyaji biashara. Kwa mujibu wa Benki ya Dunia (WB) kanda ya Afrika Mashariki ni eneo lenye uchumi unaokua kwa kasi duniani.
Hata hivyo huo ukuaji wa haraka wa uchumi unakosa nishati ya bei nafuu na ya uhakika. Idadi kubwa ya watu EAC inategemea nishati ya kuni kwa ajili ya matumizi ya kila siku nyumbani. Hali hii inaathari hasi kwa mazingira kutokana na matumizi ya kuni na mkaa yanayozidi kuongezeka kila siku. Ukosefu wa nishati ya kutosha ya umeme kunaleta hali ya mgao wa umeme kuwa hali ya kawaida katika masiha.
Wafanyabishara hulazimika kuwa na majenereta kujihami wakati umeme unapokatika kutokana na mgao. Tanzania ina kiasi cha umeme wa megawati zipatazo 1500 asilimia 20 kati hizo huunganishwa na gridi ya taifa.
Mataifa ya EAC kwa kushirikiana na wafadhili wanadhamiria kuongeza kiasi cha uzalishaji wa umeme kwa megawati 1600 ifikapo mwaka 2017. Viwango vya uzalishaji umeme kwa nchi nyingine za EAC kwenye mabano ni pamoja na Kenya (megawati 1700), Uganda (megawati 680), Rwanda (megawati 110).