Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mai Mosi) Dar es Salaam yameingia dosari baada ya madereva wa mabasi yaendayo mikoani kugoma kwa saa nane kabla ya kuendelea na safari zao, hali iliyozua kero kubwa kwa abiria waliokuwa wakielekea sehemu anuai mikoani na nje ya nchi.
Madereva hao jana katika Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani (Ubungo) walifanya mgomo wakitaka baadhi ya mambo ambayo yamekuwa vikwavyo katika shughuli zao yapatiwe ufumbuzi haraka kabla ya wao kurejea kazini.
Kwa mujibu wa baadhi ya madereva wa mabasi hayo walisema miongoni mwa madai wanayotaka kupatiwa ufumbuzi ni suala la wao kupewa mikataba na wamiliki wa magari hayo, jambo ambalo wamekuwa wakililalamikia lakini Serikali imeshindwa kuwasimamia.
Waliyataja mambo mengine yaliochangia wao kufanya mgomo ni vitendo vya kinyanyasaji vinavyofanywa na askari wa usalama barabarani vya kuwaomba rushwa na kuwaandikia adhabu kubwa kwa makosa ya kawaida jambo ambalo limezidi kuwakandamiza.
Wamedai madereva wengi hawana mikataba na waajiri wao na wamekuwa wakilipwa ujira mdogo kwa kazi wanazofanya huku wamiliki wakionesha huwalipa fedha nyingi kwa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), licha ya gharama za maisha kupanda maradufu.
“Madereva wengi hatuna mikataba ya kazi na waajiri wetu, tunalipwa ujira mdogo, hatuna bima na zinapotokea ajali sisi tunatelekezwa hata kushtakiwa huku tajir akineemeka…matajiri hao hao wamekua wakiidanganya Sumatra wanatulipa fedha nyingi, huu ni utapeli na unyanyasaji,” alisema dereva mmoja.
Hata hivyo walikubali kuendelea na safari zao baadaye baada ya viongozi wa Sumatra, Jeshi la Polisi, Madereva pamoja na baadhi ya Wamiliki wa Mabasi kufanya mazungumzo ya kutafuta muafaka. Baada ya mazungumzo hayo madereva walikubali kuondoa magari huku wakitaka kukutanishwa na wamiliki wa magari hayo Jumanne hii na kama hakitaeleweka watafanya mgomo mwingine kushinikiza madai hayo.
Magari hayo yaliondoka majira ya saa saba mchana ikiwa tayari abiria wengi wamekata tama ya kuendelea na safari zao, huku baadhi yao wakiambulia kipigo kutoka kwa askari wa kutuliza ghasia (FFU), baada ya kushinikiza warudishiwe nauli kwa viongozi wa polisi ambao walikuwa wakifanya mazungumzo ili safari zirejee.
Mgomo huo ulioanza tangu saa kumi na mbili asubuhi ulidumu kwa saa nane umewaathiri kiasi kikubwa abiria kwani wengi watafika sehemu wanazoenda usiku jambo ambalo litakuwa na usumbufu mkubwa tofauti na walivyopanga.