AMINI usiamini, tukio hili limetokea hivi majuzi. Wiki iliyopita nilikuwa katika ziara ya kikazi katika Jimbo la Kisarawe nikiwa pamoja na Mbunge wa jimbo hilo, Seleman Jafo.
Tulitembelea vijiji vingi vikiwamo Sungwi, Masaki, Chang’ombe, Mfuru, Kikwete, Boga, Msanga, Chole na Kijiji cha Kibuta.
Tukiwa katika Kijiji cha Kibuta, tuliambiwa kijijini hapo mmoja wa wapiga kura wa mbunge huyo aliyefahamika kwa jina la Abdallah Salum (67) amefanyiwa tendo la kinyama ambalo huwezi kuamini kwamba limefanywa na binadamu wenye akili timamu.
Tulielezwa kuwa, Salum ambaye ni maarufu kwa jina la Kifo, ana mke na watoto saba na kwamba waliomkata uume wake ni vijana watatu ambao walimvamia nyumbani kwake kijijini hapo na kumfanyia tendo hilo bila sababu za msingi.
Baada ya kuelezwa tukio hilo, nilitaka kujua chanzo chake na ni hatua gani zimechukuliwa kwa wahusika kwa kuwa kitendo kilichofanyika hakikubaliki katika jamii.
Nililazimika kumtafuta Mzee Kifo, baada ya dakika chache jitihada zangu zilizaa matunda kwani nilifanikiwa kuonana naye na hapo akaanza kunisimulia mkasa huo ambao ulionekana kunitisha kutokana na jinsi ulivyotokea.
Katika mazungumzo yake, Kifo anaanza kwa kueleza jinsi alivyokatwa uume huo na ni hatua gani zimechukuliwa baada ya tukio hilo ambalo anaeleza kuwa limekuwa chanzo cha kuyumba kwa ndoa yake.
“Mwanangu unajua binadamu tumeumbwa tofauti na wanyama, binadamu tuna huruma kwa huruka zetu hali kadhalika binadamu tuna akili na uelewa mkubwa kuliko viumbe wengine wote unaowafahamu.
“Lakini, nakwambia sisi binadamu ambao tuna akili kuliko viumbe wote duniani, tuna ujasiri wa kuweza kufanya matukio ya ajabu ambayo mtu akikusimulia unaweza usiamini kutokana an uzito wa tukio hilo.
“Nasema hivyo kwa sababu katika tukio hili la kwangu, awali nilikopa Sh 450,000 kwa kijana mmoja anaitwa Mbaraka wa hapa hapa kijijini kwetu.
“Wakati nakopa fedha hizo mwaka juzi, tulikubaliana nimlipe ndani ya muda mfupi, lakini, kutokana na matatizo niliyokuwa nayo kwa wakati huo, nilishindwa kumlipa ndani ya wakati jambo ambalo lilionekana kumuudhi Mbaraka.
“Nilipoona lawama zinazidi, nikajipigapiga huku na kule, nikafanikiwa kupata Sh 300,000 nikazilipa, kwa hiyo, nikabaki na deni la Sh 150,000 ambazo nazo nilitakiwa kuzilipa mapema iwezekanavyo,” anasema Kifo.
Wakati akiwa katika jitihada za kutafuta fedha hizo, anasema Mbaraka alimgeuzia kibao na kutaka amlimpe bati 20 alizokuwa nazo kama fidia ya Sh 150,000 alizokuwa akimdai, jambo ambalo yeye hakuwa tayari kulikubali kwa vile bati hizo alikuwa na shida nazo.
“Hili la kutaka nimlipe mabati 20 badala ya fedha alizokuwa akinidai nililikataa kwa sababu kama ningempa mabati hayo, mipango yangu ingeharibika kabisa.
“Kwa hiyo, nikamwomba anivumilie kidogo kwa sababu wakati huo nilikuwa katika mikakati ya kutafuta fedha hizo nimlipe ili niepukane na lawama za kila wakati kwa sababu hata jina langu alikuwa ameshaanza kulichafua hapa kijijini,” anasimulia Kifo.
Kwa mujibu wa Kifo, jitihada zake za kutaka Mbaraka aendelee kumpa muda hazikuzaa matunda kwa sababu Oktoba 22 mwaka jana alikatwa uume na vijana watatu waliomvamia nyumbani kwake majira ya asubuhi.
Anasema, vijana hao inasemekana walikuwa wametumwa na Mbaraka kwa kuwa baada ya tukio hilo, wote walitoroka na kukimbilia kusikojulikana.
“Siku hiyo ya tukio nilikuwa nyumbani kwangu majira ya asubuhi, wakaja vijana watatu, Shukuru Mwita, Paschal na Dotto, wakaniita kama wasamalia wema, nami nikatoka nje kwa sababu ni vijana ninaowafahamu.
“Nilipotoka tu, wakanikamata kwa nguvu na kunidondosha chini wakanivua nguo na kunikata uume wangu wote kisha wakakimbia na kuniacha nikipiga kelele kutokana na maumivu niliyoyapata.
“Kwa kweli sitasahau, nilivuja damu nyingi sana, nikajua sasa nakufa, lakini namshukuru Mungu amenisaidia nimepona ingawa sasa nauguza jeraha,” anasimulia
Kutokana na tukio hilo, anasema wananchi walikusanyika nyumbani kwake baada ya muda mfupi na kuamua kumpeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe ambako alishindwa kutibiwa kutokana na ukubwa wa jeraha.
“Nawashukuru sana wananchi wa Kibuta kwa sababu nilipopiga kelele, walifika ndani ya muda mfupi, wakanipa huduma ya kwanza kisha wakanipeleka Kisarawe hospitalini ambako pia madaktari walishindwa kunitibu kutokana na ukubwa wa jeraha.
“Ili kunusuru maisha yangu, walinipa barua niende Muhimbili ambako nililazwa katika Wodi ya Mwaisela kama wiki mbili hivi kisha nikaruhusiwa kurudi nyumbani,” anasema.
Pamoja na huduma aliyopata, kwa sasa anasema anasumbuliwa na mkojo kwani haupati katika mazingira ya kawaida na kwamba kila anapokojoa anahisi maumivu makali sana.
Akizungumzia hali ya ndoa yake baada ya tukio hilo, anasema imekuwa na vurugu za kila wakati kwa sababu mkewe aliyezaliwa mwaka 1970 anataka kuondoka kwa kuwa hafanyi naye tendo la ndoa.
“Mwanangu ndoa inayumba sana, nashindwa kuelewa ni njia gani niitumie ili mke wangu atulie kwa sababu kila siku ugomvi hauishi ndani ya nyumba.
“Nasema hivyo kwa sababu kosa ambalo zamani nilikuwa nikilifanya na yeye akanisamehe, siku hizi hali ni tofauti, nikifanya kosa kidogo, anakasirika, kwa kweli mambo ni magumu sana.
“Siyo hayo tu, siku hizi kesi haziishi katika ofisi ya kijiji, nikifanya kosa tu anakimbilia kunishitaki, nikifanya hivi, anakasirika, jamani, mwanangu ndoa inayumba sana na hili linaniumiza sana ingawa sina njia ya kulitatua,” anasimulia kwa unyonge.
Pamoja na maelezo hayo, mkazi huyo wa Kijiji cha Kibuta anaonyesha kutoridhishwa na jinsi Serikali ya kijiji hicho kinavyoshughurikia suala hilo kwa kuwa hadi sasa watuhumiwa hawajakamatwa.
Kwa upande wake, Mbunge wa Kisarawe (CCM), Seleman Jafo, anasema baada ya kupata taarifa hizo, alishikwa na butwaa kwa kuwa hakuamini kama binadamu wanaweza kufanya unyama wa aina hiyo.
“Mwanzoni wakati napata taarifa sikuamini, lakini kwa kuwa taarifa nilizipata kutoka kwa mtu ninayemwamini, nililazimika kuamini nilichoambiwa kwa sababu mtu huyo asingenidanganya.
“Kwa hiyo, nilichokifanya mimi ni kuwasiliana na uongozi wa Kijiji cha Kibuta kisha vyombo vya dola ikiwamo Mkuu wa Polisi Wilaya (OCD) ya Kisarawe ili kuona namna ya walivyoshughurikia tukio hilo.
“Kuhusu huyo mgonjwa, nimemwambia asiwe mnyonge, ajione ni binadamu kama binadamu wengine kwa sababu mimi niko pamoja naye na nitamsaidia kadiri ya uwezo wangu.
“Nalazimika kufanya hivyo kwa sababu wakati wa kampeni nilikuwa nikiwaahidi wananchi kuwa nitashirikiana nao katika shida na raha, kwa hiyo, kamwe sitamwacha Kifo ateseke badala yake nitakuwa naye pamoja kwa kila jambo.
“Kwa upande wa wale watuhumiwa, nadhani tuviachie vyombo vya dola vifanye kazi zake kwa sababu ndivyo vinavyojua namna ya kuwakamata wahusika na hatua gani za kisheria zichukuliwe dhidi yao pindi watakapotiwa mbaroni,” anasema Jafo.
chanzo:gazeti la Mtanzania