Watanzania:Eleweni anachokifanya Mchungaji Ambilikile Masapile

  • *Asema dawa anayotoa si kinga, ni dawa ya kuponya
  • *Asisitiza mtu akinywa dawa akapime afya baada ya siku 7

Na Masyaga Matinyi,Loliondo

Mchungaji mstaafu Masapile akiendelea kutoa dawa

KINACHOENDELEA kutokea kijijini Samunge, Loliondo mkoani Arusha si vibaya tukakiita “MUUJIZA WA KARNE,” kwa sababu ni tukio ambalo halijawahi kushuhudiwa Tanzania.

Tofauti na matukio mengine makubwa ambayo yamewahi kutokea katika Taifa letu yakiwamo Uhuru mwaka 1961 na kifo cha Baba wa Taifa mwaka 1999, sidhani kama kuna tukio ambalo limekusanya watu wengi kama hili la dawa inayotolewa na Mchungani Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Masapile.

Pia tofauti na matukio hayo mawili ambayo nimeyataja hapo juu, tukio la kijijini Samunge linahusisha gharama kubwa za usafiri na hatari nyinginezo zikiwamo ajali kutokana na ubovu wa barabara na zile za kiafya, vitu ambavyo maelfu wanaokwenda huko hawaonekani kutatizwa navyo, jambo ambalo linadhihirisha upekee wake.

Nyumba aliyokuwa akiishi kabla ya kustaafu kazi mwaka 1988 kijijini Samunge Wilayani Loliondo

Pia katika ulimwengu wa leo, mtu angetarajia kuona mtu mwenye kuweza kuvuta umati mkubwa wa watu kama ule uliopo kijijini Samunge, akiwa msomi au mjanja wa mjini kama wale wanaojiita manabii, maaskofu wazee wa upako na mitume, lakini hali ni kinyume kabisa.

Mchungaji Masapile (78) ni mtu mpole, mnyenyekevu, masikini asiye na kitu, haonekani kuwa ni mtu mwenye kupenda fedha, anamwogopa Mungu na si mtu wa mzaha hata kidogo, anajiamini, hapendi sifa wala kuabudiwa na si mbinafsi.

Ukweli huo,unadhihirisha utendaji wa Mungu pale anapotaka kufanya kitu kikubwa na kizuri kwa ajili ya mwanadamu, ambapo humtumia mtu ambaye hakuna anayeweza kumdhania.
Hata Mungu alipotaka kumleta Yesu Kristo kutukomboa wanadamu (kwa mujibu wa imani ya Wakristo), alimtumia Yohana Mbatizaji, mtu ambaye alikuwa akiishi nyikani, kwa lugha rahisi mtu wa hali ya chini kabisa.

Watu wengi naamini hawajapata fursa ya kukutana au kumsikia Mchungaji huyo, kwa hiyo ni vizuri kabla ya kuendelea makala haya nikamnukuu maelezo yake kuhusu ni nini anachokifanya kabla ya kuendelea, maelezo ambayo aliyatoa mbele ya vyombo vya habari Machi 17,2011.

Alisema; “Ni kweli ndivyo ilivyo, Mungu amenipa maono kwamba mataifa yote watakuja hapa wanaosumbuliwa na magonjwa niliyoyataja (ukimwi, kisukari, pumu, shinikizo la damu, kansa na mengineyo) kwamba watakuja kutumia dawa hapa na wala si pengine.

“Sasa nina mambo ambayo nataka kuwaambia wenzetu wanaokuja hapa hasa wale wanaowaleta wagonjwa mahututi hapa, hii si hospitali ya rufaa, watu wanakuja kabla hawajatufikia sisi wengine wanapoteza maisha ndani ya magari,

“Wengine wanakuja na dripu kitu ambacho sisi hatuna, nimejaribu kuongea hata na madaktari wengine ambao wanakuja hapa, lakini wananiambia hawawezi kumzuia mtu ambaye anataka kumchukua mgonjwa wake, lakini nimekataa hilo wasifanye hivyo.

“Serikali ijaribu kuzuia jambo hilo si jambo jema. Jingine ambalo nataka kulizungumzia na mnisaidie kuwaeleza watu, kuna watu ambao wameanza kuwaambia vijana wa huku kwetu ambao wanajua miti hiyo tunayoitumia kwamba wawachimbie, na wapo ambao wameshachimbiwa tayari kwa lengo la kwenda kutengeneza dawa.

“Sasa nawambia ya kwamba si kweli, huo ni wizi sikubali mtu yoyote mahali popote kupewa dawa na mtu kwamba mimi nimeitambua dawa hiyo, Mungu hakuagiza hivyo, naomba taifa letu lijaribu kuwatangazia mataifa mengine kuwa dawa ya aina hiyo haitakuwa dawa, hadi pale Mungu atakapoagiza vinginevyo.

“Kwa wakati huu amemruhusu mtu mmoja tu ambaye ni mimi kutoa dawa hii, nitakapochimba dawa hiyo na mwingine akachimba, Mungu ameniambia kuwa ya huyo mtu si dawa, kwa hiyo watu wasidanganywe na matapeli.

Nyumba anayoishi Mchungaji Masapile kijijini kwake

“Kuhusu masharti ya dawa hakuna, ila mimi nimeweka sharti moja, si Mungu, nawaambia watu kwamba ukitumia dawa hii basi kama wewe ni mtumiaji wa pombe usinywe siku uliyokunywa dawa na kama sharti hili lisingekuwa sawa, basi Mungu angeniambia.”

“Kwa mtu yoyote awe na imani au awe na imani ndogo tangazo langu ni moja, kwamba Mungu amesema hivi dawa yake inashika nafasi ya zile dawa alizokuwa akizitumia, lakini ni hiari ya mtu kuacha kutumia au kuendelea kutumia hadi hapo atakapopona.

“Nimesema hivi dawa nayotoa ina nguvu za Mungu, kwa hiyo inashika pahala pa dawa alizokuwa akitumia mgonjwa, sasa ni hiari ya mtu kuendelea kuzitumia au kuziacha.

“Kuhusu dawa hii kuwa kinga, hilo huwa nalitangaza kila mara kwenye semina ndogo kabla ya kuanza kazi kwamba hapa Mungu amenituma kuponya si kukinga, hii si dawa ya kinga.

“Maana kama ni dawa ya kinga hawatakuwa na shukrani kwa Mungu, anatakiwa mtu anayeumwa tumpe dawa atakapopona atamwambia Mungu ahsante,sio dawa ya kukinga.

“Nakubali dawa hii inatibu kila ugonjwa maana watu wameniletea taarifa walipopona ugonjwa fulani,wamesema hata magonjwa mengine waliyokuwa nayo yamepona, lakini pamoja na hayo sio kinga, ni ya kutibu aje mtu ambaye ni mgonjwa anaumwa.

“Kuhusu mimi kubezwa na watu nimeyasikia hayo, nasema watu hao hata kama angetokea mtu kwenye dhehebu lao akapewa uwezo na Mungu,wangempinga mtu huyo, ni tamaa kwamba kwa nini upitie kwa mtu mwingine na si wao?

“Sasa nawaambia hilo ni kosa wanamtukana Mungu. Nawakaribisha madhehebu mbalimbali waje kunywa dawa,ni kosa kubwa sana kwa viongozi wa baadhi ya madhehebu kuwakataza waumini wao kuja kunywa dawa japo wanatambua mtu huyu ni mgonjwa, lakini wanawanyima wasije kupata tiba.

“Dawa hii si kampeni ya kuongeza dhehebu, hapana, ni dawa ya kumponya mtu yoyote, unasali wapi, wewe ni dini gani au dhehebu gani, hilo simuulizi mtu yoyote.

“Nawaambia watu wote kwamba dawa haitaisha, kama ingekuwa itakwisha Mungu asingeniambia watu wa mabara yote watakuja hapa, dawa ipo waje kwa utaratibu.

“Kuhusu mazingira Serikali ina mengi ya kufanya, mfano tunahitaji kuhamia eneo ambalo Mungu amenipangia kufanya kazi, Serikali iende ikaandae mazingira pale.

“Pili mvua zimeanza, kuna uwezekano wa kutenganisha watu wa ng’ambo hii na nyingine kutokana na mafuriko, Serikali vile vile ilifikirie hilo, kama uwezo wao ni mdogo, basi waombe fedha mahali pengine ili tujengewe madaraja.”

Mtu yoyote mwenye nia njema akisoma maelezo ya Mchungaji huyo, hata kama hajawahi kumuona, atapata taswira kuwa ni mtu wa namna gani, hasa kwa wale ambao wameanza kumuita mzee huyo kuwa ni tapeli, mganga wa kienyeji na nabii wa uongo.

Juzi Ijumaa nilikuwa nikisoma habari mbalimbali kwenye mtandao wa kompyuta, nitakutana na maoni ya Mtanzania mmoja ambaye alidai kuwa waandishi wanaoandika habari za Mchungaji huyo na dawa anayotumia kutibu watu eti wanahongwa fedha kwa lengo la kupotosha umma.

Kwa bahati mbaya simfahamu mwananchi huyo, lakini kama ningekuwa namfahamu ningemshauri aende kijijini Samunge, akae, amsikilize na aone huduma anayotoa, kisha afikirie upya kuhusu maoni yake ambayo ni “very unrealistic.”

Mchungaji Mwasapile alianza kutoa dawa hiyo Agosti,2010 na kama ilivyo sasa baadhi ya wakazi wa Loliondo kwa ushuhuda wao wenyewe walimpuuza hadi pale walipoona wenzao wanaokunywa dawa hiyo wanapona magonjwa mbalimbali.

Hata ukizungumza na mzee huyo hii leo anakwambia kwa uwazi kabisa kuwa, aliwaonya watu wa eneo hilo kuwa wasichelewe kwenda kunywa dawa, kwa sababu muda si mrefu itawachukua zaidi ya siku mbili kuweza kumfikia na kupata dawa, kitu ambacho kimetimia kwa asilimia 100.

Na sasa onyo lake si kwa wakazi wa Loliondo, ila sasa Mchungaji Masapile anatoa wito kwa Watanzania kuwahi huduma hiyo, kwa sababu anasema muda si mrefu watu kutoka mabara yote watafika Loliondo kupata uponyaji, na amesema itafika kipindi itamchukua mtu muda mrefu zaidi kumfikia ili kupata dawa.

Kwa hiyo ukiangalia kwa umakini, utagundua kuwa huduma ya mzee huyo ni ya kipekee kwa sababu hata siku moja hajawahi kuitangaza kwenye vyombo vya habari au kwenye mabango kama tulivyozoea kuona, huduma yake inatangazwa na wale waliokwenda, wakanywa dawa na kupona.

Tembea nchi nzima kamwe hautakuta tangazo au bango kuhusu Mchungaji Masapile au dawa anayotoa, lakini tumekuwa tukishuhudia watu wengine wanaojiita watumishi wa Mungu wakitangaza kuwa wenye shida, wagonjwa waende mahali fulani wakaombewe na wakaponywe,lakini mwisho wa siku lengo kuu ni kuvuna pesa kutoka kwa wagonjwa na masikini bila hata ya huruma. Hilo halifanyiki kijijini Samunge.

Pia kuna watu ambao wamekuwa wakihoji kwa nini kama ni huduma yenye mkono wa Mungu iweje anachaji Sh 500 kwa kila kikombe kimoja cha dawa? Na baadhi ya wanaohoji hili ni viongozi wa dini.

Lakini jibu ni rahisi tu, manake hata huduma zinazotolewa makanisani zinalipiwa kupitia sadaka na michango mingine ukiacha zaka ambayo ni maagizo ya Mungu kuwa arudishiwe fungu la kumi.

Na ni sadaka hizo ndizo hutumika kulipa mishahara watumishi, kuboresha miundombinu ya makanisa, na kulipia gharama nyingine za watumishi na familia zao, kwa hiyo hakuna cha ajabu katika Sh 500 anayotoza Mchungaji Masapile.

Kwa mfano Sh 500 ambayo mtu analipa baada ya kunywa dawa haiendi mfukoni mwa Mchungaji huyo, Sh 200 inakwenda kwenye mfuko wa kanisa, Sh 200 ni kwa ajili ya kuwahudumia wasaidizi wake na Sh 100 ndiyo inakwenda kwake.

Lakini hata hiyo, Sh 100 ambayo inakwenda kwake haitumii, kwa sababu anasema kila kitu kuhusiana na dawa hiyo ni kwa mujibu wa maono aliyopewa na Mungu, hivyo hata hizo Sh 100 hatazitumia hadi pale Mungu atakapompa maelekezo.

Pia tofauti na watu wengine ambao wanadai kuwa Mungu amewapa uwezo wa kuponya iwe kwa maombi, dawa, kupiga kelele kama wehu au kumshika mtu kichwani na kumsukuma chini, Mchungaji Masapile ndiye pekee anayewaambia waliokunywa dawa waende kuthibitisha hospitali, kwa sababu ana uhakika na nguvu za Mungu zilizopo kwenye dawa hiyo.

Pia kwa kudhihirisha si mtu wa tamaa, wala hana nia ya kutaka sifa kwa kukusanya watu wengi zaidi, ameweka wazi kuwa dawa hiyo si kinga ya magonjwa au maambukizi, bali kazi yake ni kuponya maradhi.

Kauli yake hiyo kwanza imejaa ukweli, pia ni ya kiungwana kwa sababu miongoni mwa watu wanaokwenda Samunge baadhi yao wanakwenda kunywa dawa hiyo kama kinga ya magonjwa, ndio maana sasa hivi katika misururu ya watu utakuta yupo baba, mama na watoto. Kwa hiyo mtu ambaye si mgonjwa kijijini hapo si pahala pake.

Pia kuna wafanyabiashara wa imani ambao sasa wameanza kuingiwa hofu ya kupoteza waumini wao,lakini Mchungaji huyo anawatoa hofu hiyo kwa kutamka bayana kuwa, lengo lake si kukusanya watu kwa ajili ya kuanzisha kanisa, lengo lake kuu ni kuona watu wa Mungu wanapona na kuwa afya njema.

Kwa hiyo Watanzania na hata wenzetu wa mataifa mengine, tunapaswa kutambua kuwa Mungu yupo, ana nguvu nyingi na hakuna linaloshindikana kwake.

Pia tukumbuke kuwa, siku zote Mungu anapotaka kujidhihirisha mbele ya wanadamu hutumia watu wanyonge na wanyenyekevu, manake hata Masihi Yesu Kristo alizaliwa kwenye familia masikini ya fundi seremala, lakini alifanya matendo ya ajabu ikiwamo kutukomboa, lakini bado watu walimpuuza na kumbeza.
Mchungaji Masapile songa mbele, endelea kuponya watu na Mungu atazidi kukubariki. Amina.

source: gazeti la Mtanzania