MRADI wa Kuwawezesha Wanawake Zanzibar (WEZA) kesho Alhamisi (tarehe 24/11, 2011) utafanya maonyesho ya kibiashara na utetezi katika hoteli ya Bwawani Zanzibar yatakayowashirikisha wadau 350 wakiwemo wajasiriamali walionufaika na mradi huo.
Meneja wa Mradi wa WEZA, Rose Matovu amesema maonyesho hayo yatawapa fursa wanawake wa vijijini walionufaika na mradi wa WEZA zao kuonesha biashara zao na mbinu wanazotumia kufanya utetezi wa haki za wanawake na watoto.
Alisema Zanzibar kuna wajasiriamali wengi wanawake ambao wanatengeneza biashara nyingi nzuri lakini bado hawajatambulika na kuungwa mkono na wadau mbali mbali.
Matovu amesema wapo wanawake walionufaika na WEZA ambao wanatengeneza sabuni za karafuu, liwa, mchai chai, mwani na wengine wanasuka mikoba ya ukili na ufumaji wa vitambaa.
Amesema wengine wamepata ujuzi wa kutengeneza jamu, achari wakati wengine wanashughulika na kilimo na uuzaji wa mboga za aina mbali mbali zikiwemo mchicha, pilipili mboga, spinachi na vitunguu maji.
Kiongozi huyo wa WEZA amesema kuwa maonesho hayo ni muhimu kufanyika ili kuifahamisha wananchi wa Zanzibar kwamba uwezo wa wanawake na hivyo kuungwa mkono na wadau mbali mbali wakiwemo wanunuzi wa bidhaa na serikali.
Amesema wanawake pia wamekuwa wakitatua matatizo mbalimbali ya kijamii yakiwemo Ukatili wa Kijinsia (GBV) na kuchangia katika utoaji wa huduma za jamii jitihada ambazo zinapaswa kuungwa mkono na kila mpenda maendeleo.
Mradi wa WEZA umenufaisha watu 7,842 wengi wao wakiwa ni wanawake wa vijijini huko Zanzibar na Pemba ambao walikuwa na hali mbaya kiuchumi wakati mradi huo ulipoanzishwa miaka mine iliyopita.
Hivi sasa kwa ujumla wa kutokana na kuendesha biashara na kuweka akiba zao wameweza kukusanya jumla ya shilingi zaidi ya shilingi milioni 543.
Maonesho hayo yanafanyika kama sehemu ya kusheherekea mafanikio wakati Mradi wa WEZA kufikia tamati ambao umeanza 2008 na kuwawezesha kiuchumi na kijamii wanawake na wanume masikini katika mkoa wa Unguja kusini na Pemba kaskazini.
Mradi wa WEZA unaendeshwa kwa mashirikiano kati ya Care Tanzania, TAMWA, Umoja wa Ulaya (EU), Serikali ya Austria na Care Austria.