Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA) leo kimewakutanisha wahariri kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini kujadili ukatili wa kijinsia kwa jamii.
Hatua hii ni moja ya programu ya Kihistoria ya Siku 16 za wanaharakati kupinga ukatili wa kijinsia kwa jamii ambayo ilianzishwa tangu mwaka 1991 na Kituo cha Kimataifa cha Wanawake katika Uongozi (Centre for Women’s Global Leadership).
Akizungumza katika semina hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa TAMWA, Ananilea Nkya amesema lengo la semina kwa wahariri hao ni kuhakikisha wanafahamu mchango wa wanaume katika kupambana na ukatili wa kijinsia nchini Tanzania.
Akifafanua zaidi Mkurugenzi huyo alisema lengo lingine ni kuhakikisha wahariri wanakuwa mstari wa mbele kuanzia Novemba 23 hadi Desemba 10 kuwaamsha kiutendaji pande husika kuchukua hatua juu ya vitendo hivyo vya kikatili.
Aidha mada anuai zimetolewa kwa washiriki ili kujenga uelewa juu ya namna ya kutumia nafasi zao kwa vyombo vya habari na kuleta mabadiliko katika suala zima la ukatili wa kijinsia ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi wanawake na wanafunzi hasa wa kike.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia ni “Miaka 50 ya Uhuru: Pinga Ukatili Kuimarisha Tanzania Huru”. Taarifa hii imeandaliwa na dev.kisakuzi.com (www.thehabari.com)