Na Mwandishi Wetu
BENKI ya NIC Tanzania kwa kushirikiana na Klabu ya Lions ya Jijini Dar es Salaam wamejitokeza kudhamini mashindano ya mchezo ya Gofu ili kusaidia watu wenye matatizo ya macho.
Katika mashindano hayo benki hiyo imetoa jumla ya Dola za Kimarekani 2000 sawa na sh. milioni 3.5 za Tanzania lengo likiwa ni kuinua afya za wananchi hususani wanaosumbuliwa na matatizo ya macho.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mashindano hayo yaliyoshirikisha wachezaji zaidi ya 105, Mkurugenzi na Mtendaji Mkuu wa NIC Bank Tanzania, James Muchiri amesema ni matarajio yao udhamini huo utasaidia upatikanaji wa afya bora katika eneo wanalotoa huduma zake.
“Tunatarajia msaada huu ambao ni wa kwanza katika sekta hii ya michezo kupitia Lions Club utasaidia watu wenye matatizo wa macho katika maeneo watakayoenda kutoa huduma hiyo kama ilivyo kawaida ya wana Mzizima,” alisema Muchiri.
Mbali na hayo Mkurugenzi na Mtendaji huyo Mkuu wa NIC Bank Tanzania alisema inakadiwa kuwa zaidi ya watu milioni tatu nchini wanakabiliwa na upofu kutokana na uwezo mdogo wa kifedha, miongoni mwao wakiwemo wanafunzi.
Kutokana na hilo alisema watahakikisha wanajenga uhusiano mzuri baina yao na Lions Club katika kuunga mkono mchezo wa gofu na kuwahudumia wenye matatizo ya macho.
Nchini Benki hiyo ina matawi Harbour View Tower jijini Dar es Salaam, Mwanza and Arusha huku ikitoa huduma mbalimbali ikiwemo mikopo yenye riba nafuu.