Mtoto wa Gaddafi akamatwa, ICC yamnyemelea

Mtoto wa Gaddafi, Saif aI Islam

SERIKALI ya muda ya Libya imesema kuwa Saif al-Islam Gaddafi, mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, amekamatwa.

Waziri wa Sheria wa Serikali ya mpito, Mohammed al-Allagi, alisema kuwa Saif al-Islam alikamatwa karibu na Mji wa Ubari, kwenye Jangwa la Kusini-Magharibi mwa nchi. Inaarifiwa akijaribu kufika Niger, nchi ya jirani, ambako kaka ake mmoja amepewa hifadhi.

Watu walisherehekea katika Mji Mkuu, Tripoli, habari hizo zilipotoka.
Taarifa ya shirika la habari la Reuters inaeleza kuwa kundi la Walibya waliokuwa na hasira lilikusanyika katika uwanja wa ndege wa Zintan, ambako Saif al-Islam alipelekwa baada ya kukamatwa.

Kwa mujibu wa Reuters, watu hao waliwazuwia wakuu kumuondoa Saif al -Islam na watu wengine aliokamatwa naye. Televisheni ya Libya imeonesha picha za mtu, aliyeelekea kuwa ni Saif al-Islam.

Amekaa juu ya sofa, na vidole vyake vya mkono wa kulia vimefungwa kitambaa, yaani bendeji, lakini mbali ya hiyo, anaonesha ni mzima.
Mahakama ya Kimataifa ya Uhaini mjini Hague, ICC, inamsaka Saif al-Islam kwa mashtaka ya uhalifu wa kivita.

ICC inasema imepata thibitisho kuwa amekamatwa. Mkuu wa mashtaka wa ICC, Luis Moreno Ocampo, anasema atakwenda Libya kuzungumza na serikali ya mpito, kuhusu wapi kesi ya Saif al-Islam inafaa kufanywa.

-BBC