Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAKATI Mkutano wa tano wa Bunge ukiairishwa mjini Dodoma jana, Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa kumchunguza Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, David Jairo imeibua madudu makubwa yaliofanyika chini yake hivyo kamati kushauri achukuliwe hatua.
Pamoja na ushauri huo kamati pia imependekeza Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Katibu Mkuu Kiongozi-Ikulu, Philemon Luhanjo pamoja na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali (CAG), Ludovic Utoh wawajibishwe kutokana na kila mmoja kubainika anamakosa katika sakata zima.
Akisoma taarifa hiyo bungeni jana Mwenyekiti wa Kamati Teule ya Bunge, Ramo Mkani amesema kamati yake imebaini Jairo alichangisha fedha kinyume na sheria huku fedha hizo zikionekana kuwa na matumizi tata.
Akifafanua zaidi alisema kamati inashangaa kuona kiongozi huyo anachukua jukumu la kuchangisha fedha kwa madai zitatumika kugharamia maandalizi ya uwasilishaji wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara hiyo mwaka 2011/12 bungeni, kutoka kwa taasisi zilizopo chini ya Wizara yake.
Alisema fedha ambazo kiongozi huyo alizichangisha zilipaswa kutolewa na Hazina ambapo kufikia Juni 25 mwaka huu, wizara hiyo ilikwishapewa fedha yote za gharama za uwasilishaji wa bajeti husika, ambapo nyaraka zinaonesha ilipokea sh. milioni 171,542,000, kutoka Hazina.
Kamati hiyo imesema Waziri Ngeleja anatakiwa kuwajibishwa kwa kushindwa kubaini uozo huo uliofanyika chini yake, huku Luhanjo na Utoh wakitakiwa kuwajibishwa na Serikali kwa vitendo vya kumlinda/ kumkingia kifua mtuhumiwa dhidi ya vitendo hivyo vya matumizi mabovu ya fedha za Serikali.
“Baada ya kukamilisha uchunguzi wake kuhusu jambo hili, kamati teule ilibaini kwamba Katibu Mkuu wa wizara hiyo, hakuomba kibali cha waziri wa fedha ili kupata ridhaa ya kuchangisha,hivyo alikiuka masharti ya waraka huu,” alisema kiongozi huyo wa Kamati Teule.
“…Kamati teule ilibaini mahitaji halisi ya maandalizi ya uwasilishaji wa hotuba ya bajeti yalikuwa sh. milioni 207,042,000 ambayo Jairo aliyaridhia. Kati ya fedha hizo zilizohitajika, sh. milioni 35,500,000 zilitoka kwenye kifungu cha Project Coordination and Monitoring cha wizara. Kwa mantiki hiyo, wizara ilibaki na upungufu wa sh. 171,542,000,”
Pamoja na hayo Kamati imebaini kuwa kiasi cha fedha iliyoingizwa kwenye akaunti ya GST kwa ajili ya uwasilishaji bajeti ilikuwa sh. milioni 418,081,500, ambazo matumizi yake yalikuwa ni posho za siku tano kwa ajili ya kujikimu kwa watumishi 69, sh. milioni 32,425,000, vikao kwa watumishi 243 sh. milioni 127,820,000, licha ya Jairo kuelekeza kwamba maofisa 61 tu ndiyo walipaswa kwenda Dodoma.
Katibu Mkuu Jairo anatuhumiwa kuwaandikia barua watendaji wakuu wa taasisi nne zilizo chini ya wizara hiyo akiomba fedha kama gharama za kukamilisha maandalizi na uwasilishaji wa hutuba ya bajeti ya wizara yake mwaka 2011/12 bungeni.
“Taasisi zilizoandikiwa kuombwa michango ni Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania, (TANESCO) sh. milioni 40, Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati ya Maji na Mafuta (EWURA), sh. milioni 40, Wakala wa Umeme Vijijini (REA) sh. milioni 50 na Shirika la Maendeleo Petroli nchini (TPDC) ambazo kwa jumla zingefikia takribani sh. milioni 180,000,” alisema.
Anasema taasisi zilizoitikia maombi ya kuchangia ni tatu yaani TANESCO, REA pamoja na TPDC ambazo kwa pamoja zalichanga sh. milioni 140,000 ambazo zilitakiwa kuwekwa katika akaunti ya Geological Survey of Tanzania (GST) Na.5051000068 NMB Tawi la Dodoma.
Anaondeza kuwa taasisi ya EWURA walitaa kutoa kiasi cha fedha walichoomba, lakini badala yake iligharamia chakula cha mchana kwa siku tatu kwa sh. milioni 3,656,000 na tafrija ya Julai 18 mwaka huu, sh. 6,141,600 siku ambayo bajeti ya wizara ilitarajiwa kupitishwa. Kwa maani hiyo EWURA ilichangia jumla ya sh. milioni 9,797,600,” alisema Makani.
Ukiangalia hata kwenye nyaraka za mpango kazi na bajeti wa taasisi hizo zilizochangia, kwa mwaka wa fedha 2010/2011 ilibainika kuwa hazina kasma mahsusi kwa ajili ya kuchangia wizara iweze kuwasilisha hotuba ya bajeti yake bungeni.
Taarifa hiyo inaongeza kuwa malipo ya chakula na vinywaji kwa watumishi 169 kwa siku tano yalikuwa sh. milioni 17,480,000 na mafuta ya magari 15 yaligharimu sh. milioni 5,754,000, vifaa vya kuandikia sh.625,020 na takrima na viburudisho sh. milioni 8,000,000. Kati ya sh.milioni 225,482,880 zilizobakia,benki ziliwekwa sh. 99,438,400 wakati sh. milioni 126,044,480 ziko mikononi.
Makani alisema taarifa zilizokuwepo kwenye ofisi ya Bunge zilionesha kuwa viwango vya posho vilikuwa sh. 250,000 kwa viongozi wa Bunge, wabunge (vikao) sh.80,000, wabunge (usafiri) sh. 30,000, wakuu wa idara/kazi maalum sh. 80,000, maofisa sh. 50,000 na watoa huduma wengine sh. 20,000.
“Wakati wa kupitia matumizi ya wizara, viwango vya posho vilikuwa tofauti na maelekezo ya ofisi ya Bunge, kwa mfano wakati wabunge walilipwa sh. 110,000, mtumishi wa ngazi ya mhudumu alilipwa sh.120,000 badala y ash.20,000, wakurugenzi sh. 180,000 badala ya sh.80,000 na maofia wengine sh. 150,000 badala ya sh. 50,000,” alisema.