Na Mwandishi Wetu
SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) leo limeweka wazi majina ya viongozi wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mara (FAM), baada ya uchaguzi ulifanyika Novemba 13 mwaka huu wilayani Rorya.
Akitaja viongozi hao leo jijini Dar es Salaam kwa vyombo vya habari, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema katika uchaguzi huo uliendeshwa na Kamati ya Uchaguzi ya FAM chini ya Kamati ya Uchaguzi ya TFF wamepatikana viongozi halali.
Wambura alisema viongozi waliochaguliwa kwa kuzingatia Katiba ya FAM na Kanuni za Uchagzui za wanachama wa TFF ni pamoja na Fabian Samo aliyefanikiwa kutetea wadhifa wake wa Mwenyekiti, huku Deogratius Rwechungura akichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti.
Alisema wengine waliochaguliwa ni Mugisha Galibona (Katibu Mkuu), Samwel Silasi (Katibu Msaidizi), Evans Liganga (Mhazini), David Sungura (Mjumbe wa Mkutano Mkuu TFF), William Chibura (Mwakilishi wa Klabu) na Valerian Goroba (Mjumbe).
Wakati huo huo, Wambura amesema pambano la mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil- raundi ya mtoano kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Chad lililochezwa Novemba 15 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 78,389,000.
Akifafanua zaidi alisema mashabiki waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo walikuwa ni 29,111. Viti vya kijani na bluu ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 2,000 ndivyo vilivyovutia mashabiki wengi ambapo walikuwa 23,748 ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya mashabiki wote walinunua tiketi kwa ajili ya viti hivyo.
Aliongeza kuwa VIP A ambapo ndipo kulikokuwa na kiingilio cha juu cha sh. 20,000, jumla ya mashabiki 187 walinunua tiketi kwa ajili ya eneo hilo. VIP B ambapo kiingilio kilikuwa sh. 10,000, mashabiki walionunua tiketi walikuwa 1,181.
Viingilio vingine katika pambano hilo vilikuwa sh. 5,000 kwa VIP C ambapo waliingia mashabiki 1,678 wakati mashabiki 2,319 walikata tiketi kwa viti vya rangi ya chungwa ambapo kiingilio kilikuwa sh. 3,000.