Wachezaji 28 waitwa Kilimanjaro Stars

Kocha Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa

Na Mwandishi Wetu

KOCHA Mkuu wa timu ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), Charles Boniface Mkwasa ameteua wachezaji 28 kuunda kikosi hicho kwa ajili ya michuano ya Kombe la Chalenji inatakayofanyika Dar es Salaam kuanzia Novemba 25 mwaka huu.

Wachezaji walioteuliwa leo ni pamoja na Juma Kaseja (Simba), Deo Munishi (Mtibwa Sugar) na Shabani Kado (Yanga). Mabeki wa pembeni ni Shomari Kapombe (Simba), Godfrey Taita (Yanga), Juma Jabu (Simba) na Paul Ngelema (Ruvu Shooting).

Mabeki wa kati ni Juma Nyoso (Simba), Said Murad (Azam), Erasto Nyoni (Azam) na Salum Telela (Moro United). Viungo ni Shabani Nditi (Mtibwa Sugar), Ibrahim Mwaipopo (Azam), Nurdin Bakari (Yanga), Mwinyi Kazimoto (Simba), Haruna Moshi (Simba), Ramadhan Chombo (Azam), Rashid Yusuf (Coastal Union), Jimmy Shogi (JKT Ruvu Stars) na Mohamed Soud (Toto Africans).

Washambuliaji ni Mrisho Ngasa (Azam), Mbwana Samata (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Gaudence Mwaikimba (Moro United), John Bocco (Azam), Thomas Ulimwengu (TP Mazembe, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo- DRC), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Daniel Reuben (Coastal Union) na Nizar Khalfan (Vancouver Whitecaps, Canada).

Pambano la mchujo kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Dunia 2014 nchini Brazil- raundi ya mtoano kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Chad lililochezwa Novemba 15 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam limeingiza sh. 78,389,000.

Mashabiki waliokata tiketi kushuhudia pambano hilo ni 29,111. Viti vya kijani na bluu ambavyo kiingilio kilikuwa sh. 2,000 ndivyo vilivyovutia mashabiki wengi ambapo walikuwa 23,748 ikiwa ni zaidi ya asilimia 80 ya mashabiki wote walinunua tiketi kwa ajili ya viti hivyo.

VIP A ambapo ndipo kulikokuwa na kiingilio cha juu cha sh. 20,000, jumla ya mashabiki 187 walinunua tiketi kwa ajili ya eneo hilo. VIP B ambapo kiingilio kilikuwa sh. 10,000, mashabiki walionunua tiketi walikuwa 1,181.

Viingilio vingine katika pambano hilo vilikuwa sh. 5,000 kwa VIP C ambapo waliingia mashabiki 1,678 wakati mashabiki 2,319 walikata tiketi kwa viti vya rangi ya chungwa ambapo kiingilio kilikuwa sh. 3,000.