Tendwa atema cheche, ni juu ya vurugu za kisiasa

Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa

Na Magreth Kinabo – Maelezo

MSAJILI wa Vyama Vya Siasa nchini, John Tendwa amevitaka baadhi ya vyama vya siasa, viongozi wa vyama hivyo, wanachama na washabiki wa vyama husika kuzingatia taratibu na sheria za nchi na nyinginezo zilizowekwa.

Tendwa ametoa kauli hiyo leo Dar es Salaam kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari, kufuatia vurugu zilizojitokeza nchini ambazo zinasababishwa na baadhi ya watu hao kwa itikadi za kisiasa.

Aidha msajili huyo, amesema kuwa ni wakati mzuri wa kutenganisha mipaka ya vyama na mamlaka ya Serikali kwa kutambua kwamba ipo mihimili mitatu ambayo ni Bunge, Serikali na Mahakama, ambayo kila mmoja umepewa ukomo wake kimamlaka katika kufanya kazi.

“Vurugu hizi hazina tija kwa taifa na zinasababisha uvunjifu wa amani na kupelekea wananchi kutoshiriki katika shughuli za uzalishaji kwa kuwa muda wote wako kwenye mikusanyiko na wengine kuhofiwa kuathiriwa na matokeo ya vurugu hizo,” alisema Tendwa katika taarifa hiyo.

Aliongeza kuwa viongozi wa vyama vya siasa kuingilia uongozi na usimamizi wa mihimili hiyo ni kinyume na kufanya hivyo ni kuvunja sheria za nchi, kitendo ambacho mamlaka husika lazima zikidhibiti.

“…inapotokea mamlaka zikichukua hatua si busara kuanza kulalamika kwani kila mamlaka inao wajibu katika jamii. Hivyo basi Msajili wa Vyama Vya Siasa hayuko tayari kuvumilia hali hii ya uvunjifu wa sheria ya usajili wa vyama vya siasa ambayo vyama vyote vina wajibu wa kuzingatia katika utekelezaji wa kila siku wa shughuli za vyama vyao,” alisisitiza.

Hata hivyo ameongeza endapo chama chochote kinaona hakikutendewa haki katika jambo lolote na muhimili wowote kama Bunge, Serikali au Mahakama ni vyema kufuata sheria, taratibu za kisheria kuwasilisha malalamiko yao sehemu husika.