SBL yaalika wadau kuunga mkono udhamini michezo

Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Ephraim Mafuru (kushoto) akizungumza na vyombo vya habari leo Dar es Salaam, kulia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), Leodger Tenga.

Na Mwandishi Wetu

KAMPUNI wadhamini wakuu wa Kombe la Tusker Chalenji, Serengeti Breweries Ltd (SBL), kupitia kinywaji chake cha bia ya Tusker, imewataka wadau mbalimbali kujitokeza kusaidia juhudi za kukuza michezo nchini kwa kudhamini michezo.

Changamoto hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Masoko wa SBL, Ephraim Mafuru alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ofisi za TFF kuhusiana na mashindano ya Tusker Chalenji. Amesema wao kama wadhamini wakuu wa mashindano hayo wataendelea kuwahamasisha wadau anuai wa mpira wa miguu kuwa wazalendo kwa kudhamini michezo ili nchi iweze kufanya vizuri.

SBL ndio wadhamini wakuu wa mashindano hayo ambayo yamekuwa yakipata umaarufu kadri miaka inavyosonga mbele, na mwaka huu wametoa kiasi cha sh. milioni 823 kudhamini mashindano ya Tusker yanayotarajia kuanza Novemba 25, mwaka huu.