JK atoa pole kwa maafa ya mvua Mwanza

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

Na Mwandishi wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete ametuma salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mheshimiwa Evarist Welle Ndikilo kufuatilia maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa iliyonyesha jana ikiwa ni pamoja na kuumia kwa watu watatu, kubomoka kwa nyumba 57 na kuwaacha wakazi 100 wa Wilaya ya Ilemela Mkoani humo wakiwa hawana mahali pa kuishi.

Katika salamu zake za pole, Mheshimiwa Rais Kikwete amesema kuwa amepokea kwa huzuni habari za maafa hayo ya kuumia kwa wananchi, kubomolewa nyumba zao na hivyo kuwafanya wakose mahali pa kuishi kufuatia mvua hiyo kubwa iliyonyesha jana, Jumatatu, Novemba 14, 2011, na kusababisha kero nyingine kubwa ikiwamo ya usafiri mjini Mwanza.

“Nakutumia salamu za pole kufuatia maafa yaliyosababishwa na mvua hiyo kubwa. Kupitia kwako, naomba uniwasilishie pole zangu kwa wananchi walioumia na wale waliopoteza nyumba zao kufuatia mvua hiyo kubwa,” amesema Rais Kikwete.

Aidha, Mheshimiwa Rais ameuagiza uongozi wa Mkoa kuchukua hatua stahiki kuwaunga mkono wananchi wote ambao wameumia na wamepoteza makazi yao kufuatia mvua hiyo. “Chukueni hatua stahiki kuwasaidia waliopatwa na maafa.”