Na Mwandishi Wetu, Arusha
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) ameachiwa huru kwa dhamana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha leo baada ya kusota magereza kwa siku 14. Lema aliwasili mahakamani majira ya saa 3.15 na gari la Polisi namba PT. 1178 na kesi kuanza kusikilizwa saa 4 asubuhi.
Mbele ya Hakimu Judith Kamala, Mwendesha Mashitaka wa Serikali Haruni Matagane aliiomba mahakama hiyo kupanga siku nyingine ya shauri hilo kutajwa kutokana na upelelezi wake kutokamilika.
Naye wakili wa Utetezi, Method Kimomogolo aliieleza mahakama hiyo
kuwa Novemba 7 mwaka huu alipokea barua toka kwa Hakimu Mkazi Mfawidhi wa mahakama hiyo Charles Magesa iliyokwua na kumbukumbu namba, ikimjulisha kuwa mdhamini wa Mbunge huyo walitakwia kufika mahakamani hapo leo asubuhi hivyo kuiomba mahakama hiyo kutoa dhamana kwa Lema.
Hakimu Kamala baaada ya kupitia vielelezo vya wadhamini hao
alikubaliana na ombi hilo la wakili wa utetezi na kumwachia Mbunge
huyo kwa dhamana na kuahirisha shuri hilo hadi Desemba 14 mwaka huu kwa ajili ya kutajwa. Awali Mbunge huyo na wafuasi wake 18 walifikishwa mahakamani hapo Oktoba 28 wakikabiliwa na makosa manne huku Lema akikabiliwa na makosa matano, mahakama hiyo imeachia huru watuhumwia wote kwa dhamana.
Kombe, aliyataja makosa hayo kuwa ni njama ya kutenda kosa kinyume cha sheria ya kifungu nambari 384 na 385 cha kanuni ya adhabu, kosa la pili ni kufanya maandamano yasiyo halali ambayo yalianzia katika barabara ya mahakama ya hakimu mkazi mkoani hapa hadi kwa mkuu wa Wilaya ya Arusha, zilipo ofisi za Mbunge huyo.
Kosa la tatu linamkabili Lema peke yake ambaye anashitakiwa kwa
kuhamasisha watu kutenda kosa, ambapo anadaiwa kuwa katika eneo la
Clock Tower mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri
iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD) Zuberi Mwombeji, kinyume cha kanuni ya adhabu ya 390 na 35.
Kombe, aliieleza mahakama hiyo kuwa katika shitaka la nne
linalowakabili watuhumwia wote 19 ni kutokubali amri halali ya Mkuu wa
Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Mwombeji ambapo wanadaiwa kuwa
katika eneo la Hoteli ya New Arusha, wote kwa pamoja walijipanga na
kukataa amri iliyowataka kutawanyika, kinyume cha kifungu cha 42(2) cha sheria ya polisi.
Shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao ni kufanya kusanyiko la
watu lisilo halali, kinyume cha sheria ya polisi cha 45 na kifungu cha
14(1) na kanuni ya adhabu, wakidaiwa kuwa katika ofisi ya Mkuu wa
wilaya zaidi ya waandamanaji 100 walikataa kutii amri za Mkuu wa
Polisi wilaya ya Arusha, OCD Mwombeji ya kuwataka watawanyike.
Nje ya Mahakama hiyo wafuasi hao wakiwa wameshika matawi ya miti na majani na baadhi wakiwa wamembeba mbunge wao juu na kuelekea ofisi za CHADEMA Mkoa, zilizopo eneo la Ngarenaro, Manispaa ya Arusha.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi za CHADEMA mkoa, Lema alisema kuwa hakwenda magereza wka kukosa dhamana bali alikwenda huko ili kuonyesha namna ya kupingana na unyanyasaji wa Jeshi la Polisi wanaofanya kwa kuwabambikia kesi viongozi wa CHADEMA na wafuasi wake.
“Nimefurahia maisha ya jela kwani nimeona jinsi watu wanavyoonewa, nimeweza kufahamu mambo mengi ikwia ni pamoja na kuona baadhi ya watu wakwia wamefungwa kwa kukosa faini ya sh. 10,000 huku wengine wakiwa wamebambikiwa kesi mbalimbali,” alisema
Akimzungumizia Mkuu wa Mkoa wa Arusha Magesa Mulongo, Lema alisema kuwa Mkuu huyo ambaye ni mgeni mjini hapa hajua kiini cha mgogoro wa Arusha ambao ni uchaguzi wa meya wa Manispaa ya Arusha. Alisema kuwa kutokana na mgogoro huo kuzidi kukua ni lazima uchaguzi wa Meya wa Manispaa urudiwe ili kuondoa tofauti zilizopo.
“Tumepoteza madiwani 5, na tunajua uchaguzi ukirudiwa CCM watashinda katika kata zile hivyo uchaguzi wa Meya urudiwe, usiporudiwa tutaandamana waandae risasi na mabomu japokuwa tunajua katika uchaguzi wa Meya hatutashinda ila tunataka uchaguzi huo urudiwe kwa kufuata taratibu na sheria ili haki iweze kutendeka,” alisisitiza.
Mbunge huyo alisema nchi haina utawala wa kisheria wala kidemokrasia
kwa madai kuwa kulikuwa na mkono wa mtu ndiyo maana hakupewa “remove order”. Lema akizungumiza suala la Katiba mpya, alisema kuwa Serikali inataka kuchakachua katiba na kudai kuwa iwapo Katiba hiyo itachakachuliwa wataandamana nchi nzima bila kibali.