Pinda azindua ujenzi barabara ya Dodoma – Mayamaya

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akikata utepe kuzindua jiwe la msingi la ujenzi wa barabara ya Dodoma-Mayamaya.

*Magufuli aahidi kulipa bil. 200 za wakandarasi wanaodai muda mrefu

Na Martin Ntemo wa Wizara ya Ujenzi

WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda leo Novemba 12 amezindua rasmi ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami inayoanzia Dodoma hadi Mayamaya yenye urefu wa kilometa 43.6. Kipande hicho cha barabara ni sehemu ya barabara kuu inayoanzia mjini Dodoma kupita miji ya Kondoa, Babati, Arusha hadi nchi Kenya.

Sherehe hizi zimefanyikia katika viwanja vya Veyula nje kidogo ya Mji wa Dodoma. Barabara iliyozinduliwa pia ni kiungo cha Barabara Kuu ya Ukanda Mkuu wa Kaskazini inayoanzia Cairo nchini Misri, kupitia Tanzania hadi Cape Town, Afrika ya Kusini.

Nchini Tanzania barabara hiyo itawanufaisha wakazi wa mikoa ya Arusha, Manyara, Dodoma, Iringa na Mbeya ikiwa ni pamoja na nchi ya Zambia.

Awali akizungumza katika uzinduzi huo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi Eng. Dk. John Ndunguru alimwelezea Waziri Mkuu kuwa, ujenzi wa barabara kati ya Dodoma na Mayamaya ulianza Juni 2010 na unatarajia kugharimu sh. bilioni 42.23 huku ukipangwa kukamilika Septemba 2013.

Alisema mkandarasi anayetekeleza mradi huo ni Kampuni ya Sinohydro kutoka Jamhuri ya Watu wa China akisimamiwa na Mhandisi Mshauri Kampuni ya Norplan (T) inayoshirikiana na Kampuni ya CES ya nchini India. “Mkandarasi tayari yuko kwenye eneo la kazi na anaendelea na utekelezaji vizuri” alisema Ndunguru.

Kwa upande wake Waziri Mkuu Pinda akihutubia, alisema kuwa mafanikio haya yanatokana na umahiri wa watendaji wa Wizara ya Ujenzi na hasa Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli ambaye siku zote amekuwa imara katika kufuatilia majukumu na kusimamia shughuli za maendeleo ya Taifa kwa ujumla.

Naye Waziri wa Ujenzi, Magufuli akitoa maelezo yake, amezionya kampuni zinaolalamika kupitia vyombo vya habari kwamba wanaidai Serikali, nao wasije kuomba kazi hapa Tanzania. “Kama hutaki kuidai Serikali basi usije kuomba kazi” alisisitiza