RAIS wa Urusi Dmitry Medvedev juzi alisaini amri ya kumpiga marufuku kiongozi wa Libya Muammar Gaddafi kuingia au kusafiri kupitia eneo la Urusi.
Amri hiyo pia imewagusa watu wengine 15 wakiwamo watoto wa Gaddafi na maofisa waandamizi walio karibu naye.
Aidha fedha, mali na rasilimali za kiuchumi, ambazo familia ya Gaddafi inazimiliki au kuzidhibiti pia zimetaifishwa.
Wiki iliyopita, Rais Medvedev alisaini amri inayozuia kuiuzia Libya silaha baada ya maandamano ya kupinga utawala wa miaka 42 wa kiongozi huyo kugeuka machafuko ya umwagaji damu baina ya wapinzani na wafuasi wa Gaddafi.
Wakati huo huo, mapigano makali baina ya majeshi ya serikali na waasi yameendelea katika mji wenye mafuta wa Brega ambao pande zote zimedai kuudhibiti.
Magharibi mwa nchi majeshi ya serikali yanasonga mbele kuelekea miji inayoshikiliwa na waasi ya Zuwara na Misrata huku vikosi vingine vikielekea mji wa mashariki wa Ajdabiya, kabla ya nguvu kuelekezwa katika ngome ya waasi ya Benghazi.