Clouds Media Group wachangia Damu Dar

Baadhi ya Wafanyakazi wa Clouds Media Group wakiwa eneo la Mnazi Mmoja katika eneo la tukio la kujitolea damu leo mchana.

Na Mwandishi Wetu

WAFANYAKAZI kutoka Kituo cha Clouds FM na Televisheni ya Clouds leo wamejumuika na baadhi ya wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kuchangia damu katika Benki ya Damu, Kituo Kidogo cha Damu Salama kilichopo Mnazi Mmoja.

Zoezi hilo lililohamashishwa na Clouds Media Group limefanyika leo kuanzia mchana ambapo viongozi na wafanyakazi wamewaongoza baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam kutoka maeneo tofauti kuchangia damu.

Akizungumza na dev.kisakuzi.com mmoja wa wataalamu wa kutoa damu kutoka Kituo cha Damu Salama Mnazi Mmoja, Kanda ya Mashariki, Deo Richard alisema wao wameanza zoezi hilo tangu asubuhi na hadi saa nane mchana walikuwa tayari wamepata uniti 30 za damu.

Mtandao huu ulishuhudia wafanyakazi anuai wa Clouds FM na Clouds TV wakijitolea damu ikiwa ni mchango wao katika kuelekea maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru wa Tanzania. Radio Clouds FM pia ilikuwa ikirusha matangazo yake moja kwa moja kutoka eneo hilo, huku ikiendelea kuhamasisha wananchi hasa wakazi wa jiji kwenda kujitolea damu kusaidia maelfu ya Watanzania ambao wanahitaji damu kila uchao.

Zifuatazo ni picha za matukio kadhaa ya zoezi hilo;

Milad Ayo wa Clouds FM (kulia) akifanya mahojiano 'live' Sakina Liyoka mmoja wa watangazaji wa kampuni hiyo mara baada ya kujitolea damu. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Habari wa Clouds FM na Clouds TV, Joyce Shebe.

Mtaalamu wa kutoa damu, Deo Richard akimtoa damu Omar Waziri Mkazi wa Uwanja wa Ndege jijini Dar es Salaam alipojumuika na wana-Clouds leo kujitolea damu Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Hatibu Iddy Mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam akijitolea damu leo alipoungana na wana-Clouds Media Group.