Ugiriki yapata Waziri Mkuu mpya

Waziri Mkuu mpya wa Ugiriki, Lucas Papademos

MAKAMU wa zamani wa Rais wa Benki ya Ulaya, Lucas Papademos ametangazwa kuwa Waziri Mkuu mpya wa Ugiriki, kufuatia siku kadhaa za majadiliano. Taarifa ya kuthibitishwa kwa nafasi ya Papademos imetoka katika Ofisi ya Rais wa Ugiriki.

Taarifa zaidi zinasema kuwa viongozi wa vyama vikuu vitatu vinavyounda Serikali ya umoja wa kitaifa wamekuwa wakikutana na rais wa Ugiriki kujaribu kufikia makubaliano juu ya uteuzi huo. Waandishi wa habari wanasema Wagiriki watakuwa na imani kuwa taarifa hizi zitaleta utengamano kuwasaidia kukabiliana na janga la madeni lililopo sasa.

Papademos atahitaji kuongoza Serikali ya mpito inayoundwa, kuhakikisha nchi hiyo yenye deni kubwa inapata fedha za kuisaidia, na kuidhinisha fungu la dharura la dola bilioni 177 la kimataifa kutoka katika nchi wanachama wanaotumia sarafu ya Euro pamoja na Shirika la Fedha Duniani IMF.

“Rais, baada ya mapendekezo kutoka kwa viongozi wa kisiasa waliohudhuria mkutano, wamemtaka Lucas Papademos kuunda serikali mpya,” taarifa ya ofisi ya rais imesema, baada ya mazungumzo kati ya viongozi wa kisiasa na Papademos.

Serikali mpya itaapishwa adhuhuri ya Ijumaa, anasema ofisa mmoja wa ofisi ya rais. Papademos atachukua nafasi ya Waziri Mkuu anayeondoka George Papandreu ambaye alitangaza kuwa anajiuzulu baada ya kutaka kuitisha kura ya maoni kuhusu fungu la kusaidia deni kutoka eneo la euro.

Waziri Mkuu mpya atapigiwa kura ya kuwa na imani naye bungeni, siku ya Jumatatu, kwa mujibu wa kituo cha TV cha Serikali. Soko la hisa la Ugiriki lilipanda ghafla baada ya Papademos kuwasili katika Ikulu ya rais kujiunga na majadiliano siku ya Alhamisi asubuhi.