TIMU ya Taifa Stars ya Tanzania imewasili jana usiku mjini N’Djamena tayari kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa kesho Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura aliyoituma kwa vyombo vya habari leo, alisema timu hiyo imefikia hoteli ya Santana, na leo saa 10 jioni kwa saa za Chad itafanya mazoezi ya mwisho Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya.
Alisema tayari Kocha Mkuu wa Timu hiyo, Jan Poulsen amebadili uamuzi na kutaja kikosi kitakachoanza kuikabili Chad kesho. Poulsen amesema wachezaji watakao anza ni pamoja na kipa Juma Kaseja, Shomari Kapombe, Aggrey Morris, Juma Nyoso, Idrisa Rajab, Shabani Nditi, Henry Joseph, Abdi Kassim, Nizar Khalfan, Mrisho Ngassa na Mbwana Samata.
Akifafanua zaidi kuhusiana na mchezo huo Wambura alisema mchezo unaosubiriwa kwa hamu utachezwa kesho majira ya saa 10 kamili jioni, ambayo kwa Tanzania ni saa 12 jioni. Alisema wachezaji wote wako katika hali nzuri isipokuwa beki Erasto Nyoni ambaye ameamka leo asubuhi akiwa na malaria.
Wambura alisema waamuzi wote wanatoka Nigeria. Akiwataja alisema mwamuzi wa kati atakuwa Bunmi Ogunkolade wakati wasaidizi ni Tunde Abidoye na Abel Baba. Kamishna wa mechi ni Hamid Haddadj kutoka Algeria.
“Stars imekuja hapa na kikosi cha wachezaji 21 ambacho kitarejea nyumbani siku moja baada ya mechi kwa ndege ya Ethiopian Airlines kwa kupitia Addis Ababa, Ethiopia. Timu itawasili Novemba 13 mwaka huu saa 7.25 mchana na kwenda moja kwa moja kambini,” alisema Wambura.