Dk Slaa, Lissu mbaroni

Dk. Slaa akishuka kwenye Karandinga mjini Arusha

WAPANDISHWA KIZIMBANI KWA KOSA LA KUFANYA MKUSANYIKA USIO HALALI, MBOWE ASAKWA
Arusha

KATIBU Mkuu wa Chadema, Dk Willbrod Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu pamoja na wanachama wengine 25 wa chama hicho wamekamatwa na kupandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha kwa tuhuma za kufanya mkusanyiko usio halali.Mbali na hao, mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe ametakiwa kujisalimisha mwenyewe polisi baada ya kutoweka katika Viwanja vya NMC Unga Limited baada ya polisi kufanya operesheni ya kushtukiza kuwatawanya mamia ya wafuasi wa chama hicho na viongozi wao waliokesha hapo usiku wa kuamkia jana.

Juzi, viongozi hao wa juu wa Chadema walitangaza kupiga kambi kwenye viwanja hivyo kwa siku tatu ikiwa ni shinikizo la kutaka mahakama itoe kibali maalumu cha kumtoa gerezani Kisongo, Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema ambaye naye anatuhumiwa kufanya mkusanyiko usio halali.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa alisema jana kwamba viongozi hao walikamatwa alfajiri ya kuamkia jana baada ya polisi kuvamia mkutano huo wa mkesha.

Mpwapwa alisema jeshi hilo lililazimika kuvamia na kuvunja mkutano huo baada ya chama hicho kukiuka masharti ya kibali cha mkutano kilichotolewa na polisi kilichowaruhusu kufanya mkutano wa hadhara uwanjani hapo kuanzia saa 8:00 mchana wa juzi hadi saa 12:00 jioni.

Alidai kuwa katika tukio hilo, Dk Slaa alikutwa na bastola aina ya Walther namba T2CAR 61074-327963 ikiwa na risasi saba huku mtu mwingine aliyemtaja kwa jina la Daniel Zedekia Ongong’o naye akikutwa na bastola aina ya Pietro Berreta namba H.447577 Cat 5802, ikiwa na risasi 10 ambazo alisema wanaendelea kuchunguza uhalali wa umiliki wake na sababu za wahusika kuwa nazo eneo hilo.

“Wakati Mheshimiwa Lissu alijisalimisha mwenyewe kwa polisi, Dk Slaa yeye tulimkamata akiwa ndani ya moja ya magari yaliyokutwa uwanjani hapo na hakukuwa na purukushani yoyote wakati wa kuwatia mbaroni watuhumiwa,” alisema Mpwapwa.

Wengine waliotiwa mbaroni katika tuko hilo ni David Godfrey, Ally Hussein, Frank Chami, Stella Mushi, Francis Samwel, Paul Meena, Beatrice John, Matei Thobias, Davies Sedeka, Wilson Andrew, Abubakari Aireme, Peter Davis, Proches Blacy, John Ferdinand, Stephen Mathayo, Mohamed Mhoji, Titus Urio, Nelson Kimaro na Jimmy Everist.

Alisema jeshi hilo linaendelea kumsaka Mbowe kwa ajili ya mahojiano na hatua zaidi za kisheria. Alimuomba ajisalimishe mwenyewe kutokana na wadhifa na nafasi yake ya kiongozi wa umma. Hata hivyo, alionya kuwa iwapo hatajisalimisha, polisi watalazimika kutumia njia nyingine kumtia mbaroni.

Hata hivyo, Kamanda Mpwapwa alishindwa kueleza sababu za jeshi hilo kushindwa kuwachukulia hatua vijana wa CCM, walioandamana na kufanya mkutano wa hadhara bila kibali licha ya jeshi hilo kuyapiga marufuku.
“Pamoja na matukio haya kufanana na eneo la tukio kuwa sawa, lakini polisi tunashughulikia kila shauri kulingana na mazingira yake. Kisheria mtu huwezi kutenda kosa kwa sababu mwingine naye ametenda kosa kama lako,” alisema Mpwapwa baada ya waandishi kuhoji kwa nini Chadema wamekamatwa kwa kosa linalofanana na lililotendwa na vijana wa CCM ambao hawakuguswa?

RC atoa onyo
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magessa Mulongo ameonya kuwa vyombo vya dola havitakubali kuwaacha baadhi ya watu kuigeuza Arusha sehemu isiyotawalika akisema kuanzia sasa, yeyote atakayejaribu kuvuruga amani na utulivu kwa njia au sababu yoyote atadhibitiwa kikamilifu bila kujali cheo wala itikadi yake kisiasa.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Mulongo alisema: “Mtu yeyote atakayechezea amani na utulivu wa Arusha atakiona cha mtema kuni. Huu ni uamuzi wa kikao cha Kamati ya Ulinzi na Usalama. Hatuwezi kukubali baadhi ya watu wafanye Arusha isitawalike.”

Mkuu huyo wa mkoa ambaye ndiye mwenyekiti wa kamati hiyo, pia alizungumzia tuhuma kuwa anaingilia utendaji wa baadhi ya idara ikiwamo polisi na mahakama akisema hizo ni tuhuma zisizomnyima usingizi kutekeleza wajibu na majukumu yake kiutendaji na kuongeza kwamba, uwepo wa shughuli za kisiasa ikiwamo mikutano ya hadhara ya vyama, hauwezi kuvuruga mipangilio yake ya kazi.

Alitoa kauli hiyo baada ya juzi kudaiwa kuonekana maeneo ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha asubuhi kabla ya ombi la kutolewa kwa hati ya kumtoa Lema mahabusu, ili awekewe dhamana kukataliwa na hakimu Judith Kamara na hivyo kuzua taharuki miongoni mwa viongozi, wanachama na wapenzi wa Chadema.

“Kweli jana (juzi) nilikwenda mahakamani kulingana na ratiba yangu ambayo haiwezi kuvurugwa na uwepo wa Mbowe au shughuli zozote za kisiasa Arusha. Nilikwenda kumsalimia Jaji Mkuu ambaye ni mmoja wa wakuu wa mihimili ya dola aliyeko hapa kwa kazi za kimahakama. Sijaenda kutoa maelekezo Lema anyimwe dhamana na kusema hivyo ni dharau dhidi ya uhuru wa Mahakama,” alisema Mulongo.

Mkuu huyo wa mkoa aliwataka viongozi wa Serikali, watendaji na wale wa vyama vya siasa Arusha kujikita katika harakati za kuwaletea maendeleo wananchi badala ya kuendeleza siasa hata baada ya uchaguzi mkuu kumalizika huku akitamba kuwa pamoja na madai kuwa Arusha haitawaliki, bado anaamini mji na mkoa huo kwa ujumla uko shwari baada ya dola kuimarisha ulinzi.

Mahakamani
Dk Slaa, Lissu na wafuasi wengine 25 wa Chadema walifikishwa mahakamani jana kujibu mashtaka matatu tofauti likiwamo la uchochezi ambalo linamkabili Dk Slaa pekee.
Viongozi hao wa Chadema na wafuasi wao, walifikishwa mahakamani wakiwa chini ya ulinzi mkali wa maofisa wa polisi majira ya saa nane mchana na kesi hiyo ilianza kutajwa mahakamani saa 9:00 alasiri.

Wakili wa Serikali, Haruna Matagane alisema watuhumiwa hao wanashtakiwa kwa makosa mawili ya kufanya mkusanyiko usio halali usiku wa Novemba 7, mwaka huu na saa 12 asubuhi Novemba 8, mwaka huu licha ya kutakiwa kutawanyika na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi (SSP), Peter Mvulla.
Akisoma mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi, Devota Kamuzora, mwendesha mashtaka huyo alisema watuhumiwa hao kwa pamoja walikaidi amri halali ya Mvulla kinyume cha sheria walipotakiwa kutawanyika.

Alisema Dk Slaa anashitakiwa kwa kosa moja pekee la kutoa maneno ya uchochezi kinyume na sheria mnamo Novemba 7, mwaka huu saa 11:30 jioni.

“Tunatoa muda ifikapo saa kumi na moja jioni wanataka kumpeleka kwa ndege Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha, Zuberi Mwombeji kwa IGP Said Mwema ili wampangie wilaya nyingine ya kuhamia,” Matagane alisema akinukuu kauli inayodaiwa kutolewa na Dk Slaa.

Wakili huyo wa Serikali alisema Dk Slaa pia anatuhumiwa kutoa maneno ya uchochezi kutaka Lema atolewe Kisongo ifikapo saa kumi na jioni la sivyo kutakuwa na maandamano ya kumtoa Rais Jakaya Kikwete madarakani.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Mawakili wa utetezi, Method Kimomogoro na Arbert Msando waliomba watuhumiwa hao wapatiwe dhamana kwa kuwa yanaruhusu kufanya hivyo ombi ambalo lilikubaliwa na Hakimu Kamuzora akiwataka washtakiwa wote kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja kuweka ahadi ya kiasi cha Sh5 milioni.Watuhumiwa 20 wakiwamo viongozi walipata dhamana na kesi yao imeahirishwa hadi Novemba 22, mwaka

CHANZO: Mwananchi