Benki ya Posta yaisaidia JKT Ruvu

Mkurugenzi wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT), Brigedia Jenerali, Leila Chando (kushoto) akipokea msaada wa jezi pamoja na viatu jozi 30 toka kwa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi ikiwa ni msaada kwa timu ya JKT Ruvu vilivyotolewa na benki hiyo leo jijini Dar es Salaam. (Picha na Mpiga Picha Wetu)

Na Joachim Mushi

BENKI ya Posta Tanzania (TPB) imetoa msaada wa jezi na viatu jozi 3ยบ pamoja na fedha taslimu sh. milioni 2 kwa ajili ya Timu ya Jeshi la Kujenga Taifa -JKT Ruvu (Ruvu Stars), ikiwa ni jitihada za kuiwezesha timu hiyo kufanya vizuri katika michezo yake ijayo.

Misaada hiyo yenye thamani ya milioni 5 imekabidhiwa jana Makao Makuu ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) jijini Dar es Salaam na Mtandaji Mkuu wa Benki ya Posta nchini, Sabasaba Moshingi kwa Kaimu Mkurugenzi wa Mafunzo na Utawala wa JKT, Brigedia Jenerali Chando.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, Moshingi alisema msaada walioutoa ni utaratibu wa kawaida kwa benki hiyo kushiriki katika shughuli za kusaidia jamii katika sekta mbalimbali hasa maeneo ambayo kuna ushirikiano kati ya TPB na jamii.

Aidha alisema JKT kupitia kwa askari na wafanyakazi wake wamekuwa wakishirikiana kwa karibu na Benki ya Posta na kuzitumia huduma mbalimbali zinazotolewa na benki hiyo kama huduma ya Weka AkibaDaima Unavyopata (WADU), ambayo imekuwa ikiwanufaisha wafanyakazi wengi wa JKT.

Mkurugenzi wa Utawala na Mafunzo wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT), Brigedia Jenerali, Leila Chando (kushoto) akipokea mfano wa cheki yenye thamani ya shilingi milioni 2 toka kwa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi jana Dar es Salaam. Kiasi hicho cha fedha kimetolewa pamoja na seti ya jezi na jozi 30 za viatu ikiwa ni msaada wa timu ya JKT Ruvu kutoka kwa TPB vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 5. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Huduma kwa Wateja, Grace Nkunzi wa Benki ya Posta. (Picha na Mpiga Picha Wetu)


Pamoja na hayo ameshauri wafanyakazi hao kuitumia huduma mpya ya Benki ya Posta inayojulikana kama TPB Popote, ambayo mteja kwa kutumia simu yake ya mkononi anauwezo wa kupata huduma anuai za kibenki hata kama hayupo kwenye tawi la benki hiyo. Alisema huduma hiyo mpya mteja kwa kutumia simu ya mkononi anaweza kuhamisha fedha, kuangalia salio na kulipa bili mbalimbali za kibenki.
Akizungumza baada ya msaada huo Kocha Mkuu wa JKT Ruvu (Ruvu Stars), Charles Kilinda ameishukuru benki hiyo kwa msaada walioupata na kusema utawaongea mori ya kufanya vizuri katika msimu wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom nchini.

Aliwataka wadau wengine wa soka kuiga mfano wa TPB ili kuweza kuzinyanyua timu zingine ambazo zimekuwa zikiitaji msaada kama huo. Timu ya JKT Ruvu sasa imemaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom ikishikilia nafasi ya sita katika msimamo wa ligi hiyo.