Taifa Stars yaagwa rasmi, Pinda awapa zawadi nono!

Mwenyekiti wa Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Dioniz Malinzi (kushoto) akimkabidhi Bendera ya Taifa Nahodha wa Timu ya Taifa, Henry Jeseph (anayesalimiana na Malinzi), pembeni ya Jeseph ni Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jan Poulsen.

*Serengeti Breweries yazingua shamrashara za ushindi
*TFF, BMT wawataka wachezaji kupigana kiume

Na Joachim Mushi

KIKOSI cha Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ jana kimeagwa rasmi jioni katika Hoteli ya New Africa jijini Dar es Salaam, sherehe iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa soka, michezo pamoja na wahariri wa vyombo anuai vya habari.

Akizungumza na wachezaji kwa king’amuzi (TV), katika salamu zake Waziri Mkuu wa Tanzania, Mizengo Pinda ametoa fedha sh. milioni 10 ili kukisaidia kikosi hicho katika safari yao ya kuelekea nchini Chad kusaka ushindi.

Aidha ameishukuru kampuni ya Serengeti Breweries (SBL) kwa moyo wa kizalendo waliouonesha kwa kuidhamini timu hiyo na kuwataka wadau wengine wenye uwezo kufuata nyayo za kampuni hiyo ya bia.

Baadhi ya wachezaji wa timu ya Taifa wakiwa katika hafla ya kuagwa na kukabidhiwa bendera tayari kwa safari ya Chad

“Najua vyombo mbalimbali vina nia njema kwa timu yetu na vimeisaidia…lakini kwa namna ya pekee ningependa kuwashukuru sana wenzetu wa Bia ya Serengeti (SBL) ambao ndiyo hasa wamejitoa kuifadhili timu hii, huu ni mfano mzuri na wakuigwa kwa kweli…,” amesema Waziri Pinda.

Hata hivyo amewataka Stars kuipa umuhimu mchezo huo kwani ushindi wao ni sehemu ya mafanikio ya miaka 50 ya kusherehekea uhuru wa Tanzania.
Awali akizungumza kabla ya kukabidhi bendera kwa timu ya taifa, Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Dioniz Malinzi aliwataka vijana hao kupigana vita vya kufa na kupona kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huo.

Kutoka kushoto ni Teddy Mapunda wa SBL, Dioniz Malinzi wa BMT na Leodger Tenga wa TFF kwenye hafla ya kuagwa Taifa Stars jana New Africa Hotel.


“Nataka wote mtambue kuwa muwapo uwanjani mmebeba Watanzania takriban milioni 40 nyuma yenu…piganeni (chezeni) kufa na kupona ili mlete ushindi nyumbani. Rais ameniagiza niwaelezeni kuwa angependa mshinde na mrudi na ushindi nyumbani…,” aliongeza Malinzi.

Naye Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF), Leodger Tenga amewataka kutambua umuhimu wao kama wachezaji wa timu ya taifa na kufanya vizuri ili kuliletea sifa Taifa. Amewataka kuhakikisha wanafuata mbinu walizopewa na mwalimu wao na ikilazimika zao wenyewe ili kuhakikisha wanarudi na ushindi nchini.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa michezo wa nje na ndani ya nchi, wahariri wa vyombo anuai vya habari, wanahabari na wadau mbalimbali wa soka nchini.
mpira wa miguu