Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
UONGOZI wa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland kiliopo Norway umeahidi kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kuiongezea misaada hospitali ya Mnazi Mmoja ili iendelee kutoa huduma zaidi kwa jamii.
Hayo yalielezwa na Mkuu wa hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland Profesa Steiner Kuinsland, akiuongoza ujumbe kutoka chuo hicho wakati walipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein, Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo, Profesa Kuinsland alimueleza Dk. Shein kuwa Haukland inajivunia uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya hospitali hiyo na Zanzibar na kueleza azma ya kuipa msukumo mkubwa hospitali ya Mnazi Mmoja, kusaidia kuanzisha kitengo cha maradhi ya figo na kuijengea uwezo zaidi wa kutoa huduma.
Profesa Kuinsland ambaye pia, ni bingwa wa kutibu saratani kwa dawa alieleza kuwa Haukland pia, ina azma ya kusaidia uanzishwaji wa kitengo cha maradhi ya figo ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo kwa Daktari mmoja juu ya maradhi hayo pamoja na mashine za kusafisha damu.
Kwa maelezo ya Mkuu huyo wa Hospitali ya Haukland, Hospitali hiyo itaendelea kuipa Zanzibar na hasa hospitali ya MnaziMmoja misaada tiba juu ya maradhi ya mkojo, kutibu saratani kwa kutumia dawa, ufundishaji wa vifaa vya hospitali,elimu juu uongozi wa hospitali na ujenzi wa nyumba za madaktari.
Aidha, katika maelezo yake Profesa Kuinsland alieleza kuwa Haukland imeamua kwa makusudi kuziunga mkono baadhi ya nchi za Afrika na kutoa ufadhili ambapo tayari nchi za Ethiopia, Malawi, Sudan ya Kusini zimekuwa zikifaidika.
Kutokana na hatua hiyo Hospitali hiyo imeamua kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya ikiwa ni pamoja na kutoa mafunzo ya ‘Ufundishaji wa vifaa vya Hospitali’ kwenye Chuo cha Afya Mbweni ambapo pia wataleta walimu na kutayarisha mitaala.
Nae, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliupongeza ujumbe huo muhimu kwa ujio wao hapa Zanzibar na kueleza kuwa Zanzibar inathamini sana uhusiano na ushirikiano unaopata kutoka hospitali hiyo.
Dk. Shein pia, alitoa pongezi kwa uongozi huo kutokana na azma ya kutoa mafunzo kwa madaktari wa vitengo mbali mbali hapa Zanzibar pamoja na kuahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya afya na kueleza kuwa serikali ina azma ya kukiimarisha Chuo cha Afya Mbweni ili kiweze kutoa masomo ya kiwango cha Shahada hapo siku za mbele.
Alieleza kuwa Zanzibar imekuwa imeweka kipaumbele katika kuimarisha sekta zake zote za maendeleo ambapo juhudi kubwa pia, zimekuwa zikielekezwa katika kuimarisha sekta ya afya ambayo ndio muhimu katika maisha ya wananchi sanjari na utendaji kazi.
Pamoja na hayo, alieleza kuwa Zanzibar imo katika mikakati madhubuti ya kuanzisha kitengo cha maradhi ya figo, saratani na maradhi ya moyo na kueleza kuwa azma ya Haukland ya kuunga mkono uanzishwaji wa kitengo hicho itasaidia kufikia lengo lililokusudiwa na serikali.
Akieleza historia ya Zanzibar hapo siku za nyuma Dk. Shein alieleza kuwa Zanzibar ilipiga hatua kubwa katika suala zima la Uchunguzi wa maradhi kutokana na kuwa na madaktari bingwa hatua ambayo hivi sasa serikali imeamua kwa makusudi kuirejesha na kukiimarisha kitengo kwa Unguja na Pemba.
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na fedha nyingi zinazotumika katika kuwafanyia uchunguzi wagonjwa nje ya nchi hivyo kuwepo kwavitengo hivyo hapa nchini kutasaidia kuimarisha sekta hiyo ya afya na kuwarahisishia huduma hizo za tiba wananchi.
Mapema Dk. Jidawialieleza kuwa Hospitali ya Chuo Kikuu cha Haukland imekuwa na mahusiano ya muda mrefu na Hospitali ya MnaziMoja na kueleza kuwa hospitali hiyo imeshatoa nafasi na masomo kwa madaktari wa Zanzibar na hata hivyo bado inaendelea.
Dk. Jidawi alieleza kuwa Hospitali hiyo tayari imo katika hatua za awali za ujenzi wa nyumba ambayo ikimalizika itatumika kwa kuwaweka madaktari, wanafunzi na wahandisi wao wakati wanapokuwa Zanzibar.
Dk. Jidawi alieleza kuwa tayari ujembe huo ambao wamo Wakurugenzi wa vitengo mbali mbali vya Hospitali hiyo wameshafanya ziara kisiwani Pemba na wametembelea Micheweni, Wete na Chakechake kwa ajili ya kuangalia namna na kuweza kusaidia hospitali za kisiwani humo.
Pamoja na hayo, Dk. Jidawi alieleza kuwa Hospitali ya MnaziMmoja ina azma ya kuimarisha zaidi uhusiano na hospitali hiyo ikiwa ni pamoja na kubadishana wataalamu.