Ikulu yawasaidia wasiojiweza kusherekea Idd el Hajj

Jengo la Ikulu ya Tanzania

Na Mwandishi Wetu

VIKUNDI na vituo 14 vya watoto yatima na wenye ulemavu na wazee wasiojiweza vimenufaika na zawadi ya Sikukuu ya Idd El Hajj ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete. Watanzania jana, Jumapili, Novemba 6, 2011, waliungana na Waislam wengine duniani pote kusherehekea sikukuu hiyo.

Vituo vilivyonufaika na zawadi hizo za Mheshimiwa Rais ambazo ni pamoja na vyakula vya kuyawezesha makundi hayo kusherehekea sikukuu hiyo kwa furaha kama walivyo Watanzania wengine ni kutoka mikoa sita ya Tanzania Bara na mawili ya Tanzania Visiwani.

Vituo vilivyonufaika na zawadi hizo za Mheshimiwa Rais ni Kituo cha Watoto Kwetu cha Mbagala, Makao ya Watoto Yatima Mburahati, Yatima Group Chamazi, Temeke; VOSA Makao ya Watoto Yatima, Temeke na Makazi ya Wazee Wasiojiweza na Wenye Ulemavu cha Nunge, vyote katika Mkoa wa Dar es Salaam.

Mkoani Arusha, vituo vilivyonufaika ni Kituo cha Nkoaranga Children’s Home na Kituo cha Kikatiti Happy Watoto, Mkoani Iringa ni Makao ya Watoto Yatima Tosamaganga, Mkoani Tanga ni Kituo cha Watoto Wenye Ulemavu Irente, Mkoani Dodoma ni Makazi ya Watu Walioathirika na Ukoma Dayosisi ya Tanganyika na Mkoani Morogoro ni Makazi ya Wazee Wasiojiweza na Watu Wenye Ulemavu Fungafunga.

Vituo vilivyonufaika Tanzania Visiwani ni Kituo cha Watoto Mabaoni, Chakechake, Kituo cha Watoto Welezo, Unguja na Makazi ya Wazee Sebuleni, Unguja.

Katika kutoa zawadi hizo, Mheshimiwa Rais amewapa mkono wa Idd wote walioko katika vituo hivyo na kuwatakia kusherehekea sikukuu kwa furaha na amani kama Watanzania wengine.