Ghasia zaendelea nchini Syria

Ghasia na maandamano yanayoendelea nchini Syria.

WATU zaidi ya wanne wanahofiwa kuuwawa leo asubuhi nchini Syria, kwa mujibu wa wanaharakati wanaopinga serikali ya Rais Assad, na kwamba jana watu 27 waliuwawa.

Taarifa kutoka Mashariki ya Kati, zinasema ghasia bado zinaendelea ikiwa ni siku nne baada ya Serikali ya Syria kutangaza kuwa imekubali mapendekezo ya amani ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na kwamba itaondoa majeshi yake mitaani.

Kwa mujibu wa mapendekezo ya mpango wa Jumuiya ya nchi za Kiarabu ni kwamba ghasia zisite haraka Syria, na wanajeshi wa Serikali waondoshwe mabarabarani.

Vikundi vya upinzani vinasema tangu mpango huo kukubaliwa na Serikali siku ya Jumatano, mapiganao yamezidi katika mji wa Homs, shina la upinzani, na watu 23 waliuwawa Jumamosi.

Serikali inaripoti vifo piya, na imesema askari wake 22 wameuwawa hivi karibuni huko Homs, Dara na nje ya Damascus. Inaelekea Rais Assad anadharau mapendekezo ya Jumuiya ya nchi za Kiarabu, na badala yake ametoa mapendekezo yake mwenyewe: amesema anawapa miezi miwili wanajeshi walioasi kurejea makazini; na raia wasalimishe silaha walizonazo.

Inavoelekea baada ya siku chache Jumuiya ya nchi za Kiarabu itabidi kutangaza kuwa juhudi zao za kuleta amani Syria zimeshindwa; na huenda ikaitoa kwenye jumuiya.