Nadir Haroub aenguliwa kikosi cha Stars

Mchezaji Nadir Haroub

BEKI wa kati wa timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Nadir Haroub ameondolewa katika kikosi hicho kinachojiandaa kwa mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia dhidi ya Chad itakayochezwa Novemba 11 mwaka huu jijini N’Djamena.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania, Boniface Wambura aktika taarifa yake kwa vyombo vya habari leo amesema; Haroub ameondolewa baada ya kuumia kifundo cha mguu wa kulia (right ankle) akiwa mazoezini Novemba 5 mwaka huu.

Kwa mujibu wa daktari wa Stars, Dk. Juma Mwankemwa, mchezaji huyo hakuvunjika isipokuwa amepata mshtuko mkubwa wa kifundo hicho ambapo itamchukua wiki mbili kupona sawa sawa.

Wambura alisema kocha Mkuu wa Taifa Stars, Jan Poulsen amesema kutokana na hali hiyo Haroub hatakuwemo kwenye kikosi hicho kwa ajili ya mechi hiyo na ile ya marudiano ambayo itachezwa Novemba 15 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Poulsen amesema kwa muda uliobaki hataita mchezaji mwingine kwa ajili ya kuziba pengo la Haroub, hivyo kwa sasa atabaki na kikosi cha wachezaji 21 alionao kambini hoteli ya New Africa,” alisema Wambura.

Wakati huo huo Wambura amesema Taifa Stars itaondoka nchini Novemba 9 mwaka huu kwenda N’Djamena, Chad kwa ajili ya mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia itakayochezwa nchini humo Novemba 11 mwaka huu.

Alisema msafara wa timu hiyo utakaoongozwa na mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF, Eliud Mvella utaondoka saa 9 kamili alasiri kwa ndege ya Kenya Airways kupitia Nairobi ambapo utawasili N’Djamena saa 1 jioni ambapo Tanzania itakuwa saa 3 usiku.

“Timu itarejea nchini Novemba 12 mwaka huu kwa ndege ya Ethiopian Airlines na kwenda moja kwa moja kambini kujiandaa kwa mechi ya marudiano itakayochezwa Novemba 15 mwaka huu,” alisema Wambura.