Serikali inakamilisha mpango wa vijana kujiunga na JKT- Rais Kikwete

Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa Serikali inakamilisha mipango ya kuanzisha upya utaratibu wa vijana kujiunga na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria kama ilivyokuwa zamani.

Aidha, Rais Kikwete amesema kuwa Tanzania iko tayari kutoa uzoefu wake wa jinsi ya kuendesha JKT kwa Zimbabwe ambayo nayo inaangalia jinsi ya kuanzisha jeshi kama hilo kwa ajili ya vijana.

Rais Kikwete ameyasema hayo, leo, Jumamosi, Novemba 5, 2011, Ikulu, Dar es Salaam, wakati alipokutana na kufanya mazungumzo na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Zimbabwe Jenerali Constantine G. Chiwenga ambaye alikuwa katika ziara ya Tanzania.

Katika mazungumzo hayo, Jenerali Chiwenga amemweleza Rais Kikwete kuhusu hali ya kisiasa na kiuchumi katika Zimbabwe ikiwa ni pamoja na mchakato wa maandalizi ya katiba mpya ya nchi hiyo ambayo inafungua mlango wa kufanyika kwa uchaguzi mkuu mwingine nchini humo.

Jenerali Chiwenga pia ametumia mazungumzo hayo na Rais Kikwete kuishukuru tena Tanzania kwa mchango wake mkubwa katika mapambano ya ukombozi wa Zimbabwe.

Rais Kikwete ameitakia Zimbabwe na wananchi wake mafanikio katika mchakato wa mageuzi ya kisiasa na kiuchumi na kusisitiza kuwa Tanzania iko tayari kutoa mchango wowote ambao Serikali na wananchi wa Zimbabwe watautaka kutoka kwa Tanzania na Watanzania.
“Tuko nanyi. Tanzania iko na wananchi wa Zimbabwe. Huu ni uhusiano wa kihistoria ulioanzia kwenye makambi ya wapigania uhuru ya Kongwa na Nachingwea hadi kwenye misitu ya Mozambique mpaka ndani ya Zimbabwe yenyewe,” amesema Rais Kikwete na kuongeza. Ni uhusiano uliojengeka kwa damu ya Watanzania na Wazimbabwe,” Rais Kikwete amemwambia Jenerali huyo katika mazungumzo ambayo pia yamehudhuriwa na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi nchini, Jenerali Davis Mwamunyange.