Wizara ya Elimu kuwawajibisha wanaofaulisha kinyemela

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo

Na Janeth Mushi, Arusha

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philip Mulugo amesema Serikali ipo katika mchakato wa kuandaa waraka utakaosambazwa kwa wakaguzi wa Kanda, Waratibu wa Elimu Kata na Wakuu wa Shule za Msingi nchini, ambapo wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza watatakiwa kuwa ni wale waliofaulu kwa haki.

Naibu Waziri, Mulugo amesema hayo jana kwenye Maadhimisho ya Siku ya Walimu duniani, yaliyofanyika kiwilaya katika shule ya SOS ya wilayani hapa mkoani Arusha.

Naibu huyo amesema atawawajibisha vikali wakuu wote wa shule za
msingi ambao watawafaulisha wanafunzi na kuingia kidato cha kwanza bila kujua kusoma wala kuandika kwani kumekuwa na wimbi kubwa la wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wakiwa hawajui kusoma wala kuandika.

“Ni hatari kama mwanafunzi anakuwa amefaulu Mtihani wa Darasa la Saba lakini hajui kusoma wala kuandika, moto unakuja nitawawajibisha waalimu wakuu ambao watakwua wamefaulisha wanafunzi wa darasa la saba na kwenda sekondari huku wakiwa hawajui kusoma wala kuandika, waratibu kata na maofisa elimu ambao watafumbia macho suala hili kwani linadhalilisha Serikali kutokana na msingi mbovu wa elimu,” alisisitiza Mulugo

Akizungumzia suala la shule ambazo hazijasajiliwa aliwataka waratibu wa elimu kata kuwajibika kwa madai kuwa shule nyingi zimekwua zikiendeshwa bila kusajiliwa kutokana na waratibu watendaji wa elimu kutowajibika kuanzia ngazi za chini.

“Waratibu kama mnawajibika iweje kuwe na shule ambazo hazijasajiliwa? hayo yanatokea kwa sababu wapo wenzetu kuanzia ngazi za chini wasiowajibika na zoezi la ufungaji wa shule ambazo hazijasajiliwa siyo za nguvu za soda ni zoezi endelevu ili kudhibiti shule hizo ambazo hazijakidhi vigezo zinazosababisha kuporomoka kwa kiwango cha elimu hapa nchini,” alisema Mulugo

Akizungumzia moja ya mikakati ya kudumu kutatua kero za walimu ni pamoja na Serikali imepanga kutoa posho ya sh. 500,000 kwa
waajiriwa wapya wanaporipoti katika vituo vipya vya vitakavyoainishwa kuwa viko katika mazingira magumu.

“Walimu katika kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunza
serikali chini ya MMES II, imejipanga kujenga maabara 264, na nyumba za walimu 1200 kwa walimu nchi nzima kwa mgawanyo wa nyumba 2 na maabara 2 katika kila halmashauri huku kipaumbele kikiwa ni shule zilizo katika mazingira magumu,” alifafanua kwa waalimu hao

Kwa upande wake Katibu wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) Mkoa wa Arusha, Nuru Shemkaro aliwataka walimu hao kuwa na mshikamano na chama chao ili kuweza kutimiza majukumu na kutetea haki zao.

Aidha aliiomba Serikali kutatua changamoto zinazowakabili walimu ikiwa ni pamoja kuongezewa kwa mishahara pale wanapopandishwa madaraja ili waweze kujikimu kimaisha kwani walimu wengi wamekuwa wakiishi katika mazingira magumu kutokana na mishahara yao kwua midogo.