*Ni wa wilaya za Ludewa, Chamwino, Kondoa, Iringa na Shinyanga
Na Mwandishi Maalumu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amesema Wakurugenzi wa Halmashauri 16 nchini ambao wamekiuka makubaliano na Mahakama ya kurejesha michango ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Ametoa kauli hiyo leo Novemba 2, 2011 wakati akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Capt. (Mst.) George Mkuchika ambaye alikuwepo kwenye ufunguzi wa Mkutano wa Nne wa Wadau wa Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF) uliofanyika Hoteli ya Kunduchi Beach & Resort jijini Dar es Salaam.
Alisema anasikitisha kuona kwamba, kwa muda mrefu baadhi ya waajiri wamekuwa hawawasilishi michango ya wafanyakazi pamoja na kwamba imeshakatwa katika mishahara yao.
“Waajiri wengine huwasilisha michango hiyo ikiwa imechelewa na wakati mwingine huwasilishwa kiasi pungufu. Nataka nisisitize kuwa, kutowasilisha michango au kuwasilisha michango nje ya muda wa kisheria ni kosa kwa mujibu wa sheria. Kifungu cha 62 cha Sheria ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa, Sura 407 kinatoa adhabu ya riba ya asilimia tano kwa wanaokiuka Sheria hiyo(Defaulters)” alisisitiza.
Akifafanua zaidi alisema: “Nimepewa taarifa kuwa wapo Wakurugenzi 51 ambao tayari wamefikishwa mahakamani kwa ukiukaji huo wa Sheria. Inasikitisha pia kusikia miongoni mwao wapo wengine 16 ambao baada ya kuwekeana makubaliano nje ya mahakama wamekiuka tena makubaliano hayo.”
Halmashauri zinazodaiwa kukiuka makubaliano ni za wilaya za Ludewa, Makete, Babati, Bahi, Chamwino, Rombo, Kilwa, Kisarawe, Monduli, Longido na Kondoa. Nyingine ni Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Halmashauri ya Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga na Halmashauri ya Mji wa Kibaha.
“Waziri Mkuchika, hawa watu wote ni wa kuchukuliwa hatua za kinidhamu, kama kuna Mkurugenzi hawezi kazi tumtoe. Tafuta utaratibu wa kuwabana hawa 16, tuombe kibali HAZINA ili zikatwe katika vyanzo vyao,” alisema.
Alisema hata hao walioko mahakamani, Waziri Mkuchika awafuatilie kwani hakuna sababu ya kupoteza muda na fedha za umma kwa mambo ambayo yako wazi. “Mheshimiwa Waziri kwa hili lazima uwe mkali kweli kweli na kuhakikisha kuwa michango ya wanachama inalipwa yote na kwa wakati,” alisema.
Akisisitiza umuhimu wa kuwasilisha michango kwa wakati, Waziri Mkuu alisema ni lazima waajiri wawasilishe michango ya watumishi wao katika mifuko ya pensheni kwa wakati kwa vile kila mwajiri analazimika kufanya hivyo kwa mujibu wa sheria.
“Ucheleweshaji wowote wa ulipaji wa michango hauvumilika hata kidogo. Mimi nasema, waajiri wasiolipa michango kwa viwango vinavyotakiwa na kwa wakati lazima wachukuliwe hatua stahili kwa mujibu wa sheria. Tusiwaonee huruma wala aibu, maana kwa kufanya hivyo tunaandaa na mateso kwa wastaafu wasio na hatia,” alisema.
Napenda kusisitiza kuwa, Serikali haitakuwa tayari kuona wanachama wanaostaafu wanapata shida ya kupata mafao yao kutokana na Waajiri kutowasilisha au kuchelewa kuwasilisha michango yao.
Mapema akitoa taarifa ya Mfuko wa Pensheni wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mkurugenzi Mkuu wa LAPF, Bw. Eliud Sanga alisema mfuko huo umekuwa ukiimarika kila mwaka kwani umeweza kuongeza idadi ya wanachama kutokana na ubora wa mafao ya pensheni yanayotolewa, huduma ya haraka na fursa walizopewa watumishi wapya kupitia Sheria ya Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii nchini inayowaruhusu wafanyakazi wapya kuchagua mifuko wanayotaka kujiunga nayo.
“Katika mwaka wa Fedha wa 2010/11 LAPF iliweza kuandikisha wanachama 7,688 na hivyo kufikisha jumla ya wanachama hai 80,529 ilipofika Juni, 2011. Matarajio ni kufikia wanachama 90,726 ifikapo mwisho wa mwaka wa fedha wa 2011/12,” alisema.
Pia alisema ukusanyaji wa michango ya wanachama umeendelea kukua kutokana na jitihada zilizofanywa katika kuongeza wanachama, makusanyo ya kila mwezi pamoja na uamuzi wa Serikali wa kuongeza mishahara kwa watumishi wake.
“Katika mwaka wa fedha wa 2010/2011 LAPF iliweza kukusanya sh. bilioni 75.5 ikilinganishwa na sh. bilioni 54.24 zilizokusanywa katika mwaka wa fedha wa 2009/2010. Katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Mfuko unategemea kukusanya sh. bilioni 87.5 sawa na ongezeko la asilimia 15.8,” aliongeza.