Na Mwandishi Maalumu
KITUO cha wasiojiweza cha Kimbangulile Support Group kimesema kinahitaji jengo kwa ajili ya ofisi na darasa kwani kwa muda wa miezi sita sasa hawajaweza kufundisha watoto 18 kati ya 64 wanaowahudumia katika kituo hicho.
Mwenyekiti wa kikundi hicho, Bi. Leokardia Mchau ametoa ombi hilo mwishoni mwa wiki wakati wafanyakazi wa kampuni ya DataVision International Limited walipotembelea kituo hicho na kutoa msaada wa vifaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vifaa vya malazi.
Kituo hicho cha Kimbangulile Support Group kipo kata ya Mianzini, eneo la Mbagala Rangi Tatu, nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
“Watoto tunaowahudumia hawalali hapa lakini wanakuja kujifunza kila siku, kuna watoto wanne wanaoratajia kufanya mtihani wa darasa la nne mwezi huu, pia wako watoto 10 ambao wataingia darasa la kwanza mwakani na wengine wanne ambao ni walemavu wa viungo; wote hawa tumeshindwa kuwafundisha ipasavyo,” alisema Bi. Mchau.
Akizungumzia kuhusu tatizo la darasa, Bi Mchau alisema hawajaweza kuwafundisha vizuri watoto hao kutokana na uamuzi wa mwenye nyumba waliyokuwa wakiitumia kuamua kupangisha chumba kilichokuwa kikitumika kama darasa.
Akifafanua kuhusu mahitaji ya kituo hicho, Bi. Mchau alisema wana watoto 10 ambao ni walemavu; mmoja anahitaji mguu wa bandia, mwingine ana matatizo ya macho hawezi kuona, yuko mwingine ambaye ni bubu na mwingine mmoja ana matatizo ya mifupa haikui. Pia wana watoto wenye utindio wa ubongo na bubu mmoja.
“Pamoja na yote hayo, tuna watoto wawili ambao wamefukuzwa shule kwa kukosa ada. Mmoja yuko kidato cha kwanza na mwingine yuko kidato cha pili… tunaomba wasamaria wema watusaidie kubeba mzigo tulionao,” aliongeza.
Akijibu baadhi ya maombi yao, Meneja Masoko na Mahusiano wa kampuni hiyo, Bi. Teddy Qirtu alisema wanaridhishwa na maendeleo ya kikundi hicho ikilinganishwa na hali ilivyokuwa Aprili, 2011 walipowatembelea mara ya kwanza. “Tunafurahi kuona juhudi za walezi na walimu kwani kuna maendeleo kwa watoto hawa hasa kielimu…,”
Alisema kampuni hiyo itawasaidia kulipia kodi ya vyumba watakavyopangisha na kuongea na uongozi wa shule iliyowafukuza watoto hao wawili. Pia aliahidi kumsaidia mtoto Fatuma ambaye anahitaji mguu wa bandia.
Wafanyakazi wa kampuni ya DataVision International Limited walitembelea kituo hicho mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya mfumo wa kuendeleza jamii (growing people) na kutimiza wanayoyasema (walking the talk) ambao kampuni hiyo imejiwekea chini wa mpango wake wa huduma kwa jamii (Corporate Social Responsibility -CSR).
Pia walitoa vifaa mbalimbali vikiwemo vyakula na vifaa vya malazi vyenye thamani ya sh. milioni 1.08. Vifaa hivyo ni vyandarua 20 na mashuka 80 vyenye thamani ya sh. 360,000. Vingine ni kilo 100 za sukari, kilo 100 za mchele, kilo 100 za unga wa mahindi, kilo 100 za maharage, katoni 14 za sabuni, katoni nne za juisi na katoni tatu za biskuti vyote vikiwa na thamani ya sh. 720,000.