Na Janeth Mushi, Arusha
MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema na
wafuasi wenzake 11 wamesweka rumande baada ya kushindwa kutimiza
masharti ya dhamana dhidi ya kesi inayomkabili ya kufanya
maandamano na mkusanyiko bila kibali.
Shauri hilo lenye namba 437 la mwaka 2011, Mbunge huyo na wafuasi wake 18 wote kwa pamoja wamefikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Arusha, mbele ya Hakimu Judith Kamala, mwendesha mashtaka wa Serikali, Augustino Kombe alidai mahakamani hapo kuwa watuhumiwa wote walitenda makosa hayo mnamo Oktoba 28 mwaka huu.
Kosa la kwanza ambalo linawakabili watuhumiwa wote ni kula njama ya
kutenda kosa kinyume cha sheria ya kifungu namba 384 na 385 cha kanuni ya adhabu, kosa la pili likiwa ni kufanya maandamano yasiyo halali ambayo yanadaiwa ikuanzia katika barabara ya mahakama ya hakimu mkazi mkoani hapa hadi kwa mkuu wa wilaya ya Arusha.
Kombe aliieleza mahakama hiyo kuwa katika maaandamano hayo ambayo walikuwa waandamanaji zaidi ya 100 ambayo yalifanyika kinyume cha kifungu cha sheria cha 74 (1) na kifungu cha 75 cha sheria na kiyume cha sheria ya polisi kifungu cha 45.
Alidai kuwa kosa la tatu linamkabili Lema peke yake ambaye
anashitakiwa kwa kosa la kuhamasisha watu kutenda kosa, ambapo
anadaiwa kuwa katika eneo la Clock Tower mbunge huyo alihamasisha watu kujipanga na kukataa amri iliyokuwa imetolewa na Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD) Zuberi Mwombeji, kinyume cha kanuni ya adhabu ya 390 na 35.
Shtaka la nne linalowakabili watuhumiwa hao ni kutokubali kutii amri
halali ya Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Arusha (OCD), Mwombeji ambapo
wanadaiwa kuwa katika eneo la Hoteli ya New Arusha, wote kwa pamoja
walijipanga na kukataa amri iliyowataka kutawanyika, kinyume cha
kifungu cha 42 (2) cha sheria ya polisi.
Alisema kuwa shtaka la tano linalowakabili watuhumiwa hao ni kufanya kusanyiko la watu lisilo halali, kinyume cha sheria ya polisi cha 45 na kifungu cha 14(1) na kanuni ya adhabu, wakidaiwa kuwa katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, wanaodaiwa kukataa kutii amri za Mkuu wa Polisi wilaya ya Arusha, OCD Mwombeji ya kuwataka watawanyike.
Kombe alisema kuwa upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo unaendelea ambapo alimwomba Hakimu huyo kupanga tarehe ya kutajwa kwa kesi hiyo. Watuhumiwa hao ni Lema, Joseph Simon, Dina Kamtoni, Musa Mwakilema, Jafari Samweli, Juliana Lukumay, Gerald Majengo, Leonard Kiologo, Frank Daniel, Kelvin Simon na Hassan Mdigo.
Wengine ni pamoja na Lomayan Nasi, Rashid Shumbeti, Amedeus Chami, Daud Hamza, Meshack Betuel, Hamad shaban, Bahati Daud na Richard Mollel.
Kati ya watuhumiwa hao 19 walioweza kukidhi matakwa ya dhamana na
kuachiwa huru na mahakama hiyo kwa dhamana ni Dina Anthony, Gerald Majengo, Hassan Mdigo, Lomayan Nasi, Rashid Shumbeti, Daud Hamza na Bahati Daudi. Watuhumiwa wote walikana kutenda makosa kwa nyakati tofauti na Hakimu Kamala kuihairisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu itakapotajwa tena.
Aidha Mbunge huyo anakabiliwa na mashitaka mengine katika MAhakama hii ambapo yeye na baadhi ya viongozi wa juu wa Chama Chake wanakabiliwa na kesi ya kufanya maandamano na kusanyiko pasipo kibali januari 5 mwaka huu wakati katika mahakama Kuu akiwa anakabiliwa na Kesi ya kupingwa matokeo ya Uchaguzi iliyofunguliwa na wapiga kura watatu wa Jimbo la Arusha mjini.