MECHI ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya timu maarufu za Yanga na Simba iliyochezwa Oktoba 29 mwaka huu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam imeingiza sh. 337,537,000.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana kwa vyombo vya habari kutoka TFF, inasema watazamaji waliokata tiketi kushuhudia mechi hiyo walikuwa 53,366 ambapo kiingilio kilikuwa sh. 5,000, sh. 7,000, sh. 10,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 kwa VIP A.
Akifafanua zaidi Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura amesema baada ya kuondoa gharama za mchezo na Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ambayo ni sh. 51,488,694 na gharama za awali za mchezo sh. 27,405,250 kila timu ilipata sh. 77,592,916.
“Mgawo mwingine ulikwenda kwa uwanja (sh. 25,864,305), TFF (sh. 25,864,305), Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu- FDF (sh. 12,932,152), gharama za mchezo (sh. 25,864,305), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam- DRFA (sh. 10,345,722) na Baraza la Michezo la Taifa- BMT (sh. 2,586,430),” alisema katika taarifa hiyo.