Na Mwandishi wetu, Los Angeles, CA
JUMUIYA ya Watanzania kunisi mwa California ilikutana siku ya Jumamosi jijini Culver City na kujadili masuala mbalimbali kwa maendeleo ya Jumuiya na Tanzania kwa ujumla. Jumuiya hiyo, ambayo imepata uongozi mpya hivi karibuni chini ya Mwenyekiti Bi. Rabia Dahal iliweza kujadili mfuko wa chama, umuhimu wa Wanajumuiya kushiriki katika shughuli za Jumuiya, na mipango na shughuli za chama.
Katika kuonyesha msisitizo kwenye mipango na shughuli za chama, Bi. Namstasha Bunting, alizitambulisha rasmi kamati mpya za jumuiya, zikiwemo Kamati ya Masuala Endelevu (Resource Center Committee), Kamati ya Biashara na Fedha (Business and Fundraising), na Kamati ya Utamaduni, Burudani na Michezo (Culture, Entertainment and Sports). Kamati hizi zimekusudiwa kuongeza ushirikiano miongoni mwa Wanajumuiya, na pia ushirikiano wa Jumuiya na Watanzania waliopo Tanzania na kwingineko ulimwenguni.
Ajenda kuu ya mkutano ilikuwa ni kuhimiza Watanzania waliopo kwenye ukanda huu wa kusini mwa California kushiriki kwa hali na mali katika shughuli za Jumuiya, ili kuiwezesha Jumuiya kufikia malengo iliyojiwekea. Mkutano ulimalizika kwa Wanajumuiya kujumuika pamoja kwa vinywaji na vyakula vya Kitanzania, kama Maandazi, Chapati, Tambi za nazi, na mapochopocho mengine kedekede!
Kwa picha zaidi za kikao hicho, tafadhali bofya hapa: http://www.thehabari.com/matukio/jumuiya-ya-watanzania-kusini-mwa-california-yakutana-2