Uingereza yaipiga ‘nyundo’ Serikali ya Tanzania

Andrew Mitchell

YATOA ASILIMIA 30 KWENYE FUNGU LA BAJETI

SERIKALI ya Tanzania imepata pigo kiuchumi baada ya Uingereza kupunguza msaada wake katika fungu la bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 kwa asilimia 30, Mwananchi Jumapili limebaini.

Hatua hiyo ya Uingereza kupitia Idara ya yake ya Maendeleo ya Kimataifa (DFID), imekuja wakati nchi wahisani zinazochangia bajeti ya serikali (GBS), zikisema zitapitia misaada ya fedha wanazotoa ili kujua kama serikali imefikia malengo yaliyokusudiwa. Jumla ya Washirika wa Maendeleo (DPs) 12 wanasaidia bajeti ya Tanzania, ambapo kwa mwaka huu wa fedha, nchi hizo zilitoa kiasi cha Dola 453 milioni.

Hata hivyo, katika mchango wao wa bajeti ya mwaka huu wahisani wamezuia kiasi cha Dola 100 milioni (karibu Sh170bilioni) ambazo zitatolewa iwapo nchi hizo zitaridhishwa na utendaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali. Katika mwaka wa fedha 2010/11 nchi hizo zilitoa Dola 534 milioni (karibu Sh907.8 bilioni) kuchangia bajeti ya serikali.

Hatua ya kuzuiwa kwa kiwango hicho cha msaada wa Uingereza kwenye bajeti inatokana na serikali kushindwa kusimamia vizuri masuala mbalimbali, kubwa ikiwa ni mazingira ya uwekezaji na kupambana na umasikini, kwa mujibu wa Waziri wa Maendeleo ya Kimataifa wa Uingereza, Andrew Mitchell. Mitchell katika barua yake ya Agosti 3, 2011 kwenda kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Masuala ya Uchumi ya Bunge la Mabwanyenye la Uingereza (House of Lords), amesema mawaziri wa Uingereza na serikali yake kwa ujumla wamekuwa wakisisitiza Tanzania kuimarisha mazingira ya kufanya biashara kama njia muafaka ya kupunguza umasikini.

“Hatua za kuhakikisha Tanzania inakuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji zimehusishwa katika kitengo cha ufuatiliaji wa misaada kwenye bajeti unaotolewa na Uingereza,” “Mwaka huu nimepunguza msaada wa Uingereza kwenye bajeti ya Tanzania kwa asilimia 30, kuonyesha kuwa tuko makini katika hili,” alisema Mitchell katika barua hiyo.

Mei 2010, Mitchell, aliiagiza Tume ya Mapitio ya Misaada (Bilateral Aid Review) kuchunguza kwa makini nchi ambazo DFID inafanya kazi kupitia programu za Uingereza za moja kwa moja za nchi na kanda. Mapitio hayo kwa mujibu wa mpango kazi wa DIFD nchini wa mwaka 2011 – 2015, yalitazama njia bora ambazo Uingereza inaweza kutumia kupambana na umaskini na kuhakikisha unakuwepo ufanisi wa kila fedha ya nchi hiyo inayotumika. Machi 2011, matokeo ya mapitio hayo yalitangazwa ambapo pamoja na mambo mengine, walifanya mapitio ya misaada inayotolewa kwa nchi mbalimbali. “Mapitio hayo yalifanya tubadili kidogo mtazamo wa programu zetu na yametufanya tulenga nchi chache zaidi ili misaada yetu iende pale ambapo italeta tofauti na pale palipo na mahitaji makubwa,” inasema sehemu ya mpango kazi huo wa DIFD wa miaka mine kuanzia 2011.

Mapitio hayo pia yamependekeza DFID Tanzania kupunguza kutumia mfumo wa kupitisha msaada kwenye Bajeti ya Serikali (General Budget Support), kama tathmini ya programu ya nchi ya mwaka 2010 ilivyoshauri. “Tathmini hii ilionyesha kuwa katika hali ya sasa, kupitisha msaada kwenye bajeti ya serikali si njia yenye ufanisi zaidi ya kuwasilisha matokeo ya misaada yetu na ilipendekeza tupunguze matumizi ya mfumo huo.” Naibu Waziri wa Fedha Akizungumza na Mwananchi Jumapili kwa njia ya simu, Naibu Waziri wa Fedha, Pereira Silima, alisema uamuzi huo wa Uingereza hautaiathiri serikali kwani ilishapanga bajeti kulingana na kiasi cha fedha walichokwisha fahamu kuwa watakipata.

“Unajua tunapopanga bajeti, tunajua wafadhili wanatoa nini, kwa hiyo taarifa tunapoipata kuwa fulani atapunguza, inakuwa iko nje ya bajeti yetu,” alisema Silima. Alifafanua kuwa kiasi kilichoingizwa kwenye bajeti kwa mwaka wa fedha 2011/12 ni kile ambacho kiliahidiwa kutolewa na kuongeza kuwa bajeti haitadhurika kwani kama ni kutafuta njia mbadala, serikali ilishafanya hivyo tayari. Alikiri kuwa taarifa ya kupunguzwa kwa kiasi hicho cha fedha kwenye mchango wa bajeti walishaipata kwenye vikao vya awali vya kupanga bajeti na kuongeza: “Kuna wakati tunakuwa na vikao vya kuulizana ambapo kila nchi husema kile ambacho itachangia katika bajeti ya mwaka husika.”

Alipoulizwa kuwa kama Uingereza ilitoa sababu ya kupunguza fedha hizo, Silima alisema nchi hiyo ilibadilisha utaratibu kulipoingia serikali mpya. “Unajua serikali ni nyingine kwa hiyo zile taratibu zilibadilishwa na walipunguza nchi nyingi katika orodha ya nchi walizokuwa wakizisaidia,” alisema Silima. John Mnyika Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika aliitaka Uingereza kuweka wazi sababu za kupunguza misaada kwani kuna mambo mengi ambayo nchi wahisani wa maendeleo hawaridhiki nayo lakini hawaweki wazi. Aliongeza kuwa wadau wa maendeleo hawaridhiki na jinsi Serikali ya Tanzania inavyoshughulikia ufisadi, hususan suala la EPA.

“Baada ya EPA kujadiliwa bungeni, Serikali ya Tanzania ilikubaliana na wahisani kutengeneza mpango kazi wa kushughulikia ufisadi wa EPA, sasa hawaridhishwi na jinsi hatua zinavyokwenda,” alisema Mnyika. Aliongeza kuwa wahisani hao bado hawaridhishwi na jinsi serikali inavyoshughulikia mianya ya ubadhilifu wa fedha za bajeti ndani ya serikali. “Sehemu kubwa ya pesa za bajeti zinaishia mikononi mwa mafisadi badala ya kuwafikia wananchi na kuendeleza miradi yao,” aliongeza.

Mnyika ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo, aliongeza kuwa sababu nyingine ya Uingereza kupunguza misaada yake kwa nchi nyingi, ni mgogoro wa kiuchumi kwa nchi za ukanda wa Ulaya hususan tatizo la madeni linalozikabili nchi hizo hivi sasa. Alishauri kupunguzwa kwa matumizi yasiyo ya lazima ya serikali ili kufidia upugufu huo.

CHANZO: Mwananchi