Serikali inauwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi wake tofauti na ilivyokuwa kabla ya Uhuru- Waziri Mkulo

Kutoka kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Posta Tanzania (TPB), Sabasaba Moshingi akizungumza jambo na mmoja wa maofisa wa Benki Kuu, Lenny Kissarika wakati wa sherehe za uzinduzi wa Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru ya Wizara ya Fedha katika viwanja vya Mnazi Mmoja. (picha na Joachim Mushi)

Na Joachim Mushi

WAZIRI wa Fedha wa Tanzania, Mustafa Mkulo amesema Serikali kwa sasa inauwezo mkubwa wa kuwahudumia wananchi wake ukilinganisha na kabla ya nchi kupata uhuru. Hata hivyo amesema licha ya minong’ono ya lawama iliyopo kwa baadhi ya watu, hali ya maisha ya Watanzania ilivyo leo haiwezi kulinganishwa na ilivyokuwa wakati nchi inapata uhuru wake.

Waziri Mkulo amesema hayo leo jijini Dar es Salaam alipokuwa akifungua rasmi Maonesho ya Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 50 ya Uhuru ya Wizara ya Fedha katika Viwanja vya Mnazi Mmoja.

Amesema tangu nchi ipate uhuru zipo jitihada mbalimbali ambazo zimekuwa zikifanywa na Serikali kuhakikisha inapunguza hali ya umasikini kwa Wananchi, ambazo tayari zimeanza kuonesha mafanikio.

“Hali ya maisha ya Watanzania ilivyo leo sivyo ilivyokuwa wakati tunapata uhuru. Watu wengi wanapata huduma za kijamii kama vile, elimu, huduma za afya pamoja na barabara,” alisema Waziri Mkulo akihutubia kabla ya kufungua maonesho hayo.

Aidha ameongeza kuwa uchumi wa Tanzania kwa ujumla umeonesha mafanikio ya kuvutia tangu uhuru, ingawa kuingia kwa mdororo wa uchumi na fedha duniani umechangia kuathiri maendeleo ya ukuaji wa sekta binafsi hususan kupungua kwa mikopo iliyokuwa ikitolewa na sekta hiyo.

Pamoja na hayo amesema Tanzania imekuwa na mikakati anuai tangu nchi ipate uhuru, ya kuhakikisha inaboresha kilimo kama vile ukulima wa kisasa, vijiji vya ujamaa, siasa ni kilimo, chakula ni uhai, pamoja na kilimo cha kufa na kupona.

“Ili kupunguza nusu ya umasikini wa chini ya dola moja kwa siku kufikia mwaka 2015, lengo ni kukuza kilimo kwa asilimia 10 kwa mwaka tofauti na asilimia 3.3 ya sasa. Ili kufikia malengo hayo Serikali imeongeza kasi ya mapinduzi ya kilimo kwa kuzindua ‘Kilimo Kwanza’…,” alisema Mkulo.

Maonesho hayo yanashirikisha taasisi mbalimbali zilizo chini ya Wizara ya Fedha ikiwemo Benki ya Posta Tanzania (TPB), Twiga Bancorp, Bodi Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAAA), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na taasisi nyingine anuai zinazofanya kazi chini ya wizara hiyo. Maonesho hayo yalioanza Oktoba 24 yanatarajiwa kufungwa Oktoba 30.