Na Mwandishi Wetu, Arusha
MAHAKAMA Kuu Kanda ya Arusha, leo imeshindwa tena kuanza kusikiliza kesi ya kupinga matokeo ya Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA), baada ya watu kufurika katika chumba cha Mahakama.
Kesi hiyo namba 13 iliyofunguliwa na wapiga kura watatu Mussa Mkanga, Agnes Mollel na Happy Kivuyo – ambao kwa pamoja wanaiomba mahakama kutengua ushindi wa Lema kwa madai ya kukiuka sheria wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu uliopita.
Kesi imekwama kusikilizwa kutokana na wingi wa watu waliokuwa wamehudhuria mahakamani hapo.
Aidha Jaji huyo alikubaliana na hoja zilizokuwa zimetolewa na Mawakili
wa wadai kuwa kesi hiyo haiwezi kusikilizwa kutokana na wingi wa watu
waliokuwa katika chumba cha mahakama hiyo.
“Nakubaliana na hoja za mawakili hao kwani hali hairidhishi kuendelea
usikilizwaji wa kesi hii, hata hali ya hewa huku ndani inaelekea
kuboreka milango imefungwa, hii ni hatari kwa hali ya usalama wa
Jaji, watendaji wa mahakama na hata wasikilizaji,” alisema Mujulizi
Alisema kuwa iwapo kutatokea jambo la dharura ndani ya chumba hicho na watu kutakiwa kutoka nje ingekuwa ni vigumu kutokana na wingi watu waliokuwemo.
Awali kesi hiyo iliyokuwa ianze kusikilizwa jana saa tano asubuhi
ilishindikana hadi ilipofika saa 6;30 mchana, kutokana na wingi watu
waliokuwa katika chumba hicho kusikiliza shauri hilo, ambapo yalizuka
malumbano ya zaidi ya dakika 40 baina ya watu hao na mawakili
waliokuwa wakitaka watu waliokuwa wamesimama watoke nje ya chumba hicho.
“Ili tupate uwezekano wa kesi yetu kuendelea waliosimama watoke nje
kwani itakuwa ni vigumu kusikilizana kwa leo naomba tusaidiane ambaye hajapata mahali pa kukaa asimame nje ya Chumba cha Mahakama,” Alisema wakili Method Kimomogolo anayemtetea Mbunge huyo,ambaye alipingwa vikali na watu hao.
Aidha ilipofika majira ya saa 6;08 mchana Wakili anayewakilisha upande
wa wadai Alute Mughwai,aliwaeleza wananchi waliokuwa katika chumba
hicho cha mahakama kuwa iwapo hawatapungua nao hawataendelea na kesi hiyo, ambapo wananchi hao waliamua kukaa chini ndani ya chumba hicho hali iliyosababisha chumba hicho kutokuwa na nafasi. “Kama hampungui tunaenda kwa Jaji kuendelea na shughuli nyingine,” alidai Alute.
Aidha Jaji huyo alilazimika kuingia mahakamani hapo majira ya saa 6;30
mchana huku watu wakiwa wamejaa katika milango yote miwili ya kuingia ndani ya chumba hicho, madirishani huku wengine wakiwa wamekaa chini.
Wakili wa Upande wa wadai Mughwai, aliieleza mahakama hiyo kuwa upande wa wadai uko tayari kwa ajili ya shauri hilo kuanza usikilizwaji wa awali ila kutokana na wingi wa watu hawataweza kufanya kazi yao kwa ufanisi.
“Mheshimiwa Jaji chumba cha mahakam hakiko tayari wka ajili ya
shughuli hiyo watazamaji wamejaa,watenja wangu wako nje kwa sababu
viti vilivyokuwa vimetengwa kwa ajili yao vimejaa watu, kizimba ambacho walipaswa kutolea ushahidi naki kumejaa watu, milango imefunguliwa ila watu wamehaa hewa ya kuvuta sasa imeanza kuleta shida,” alidai wakili huyo.
Mughwai alimwomba Jaji huyo kabla ya shauri hilo kuendelea, atoe mwelekeo wa namna ya mahakama itakavyoweza kusikiliza kesi hiyo.
“Mahakama ni mhimili wa tatu wa dola na taratibu za mahakama zinapaswa kufuatwa, hata bungeni kuna taratibu za kufuata Ikulu hivyo hivyo mnaingia kwa utaratibu mnaopewa na mamlaka husika, hatuwezi kuendelea katika mazingira haya,” alisema wakili huyo
Kwa upande wake wakili wa Serikali anayemuwakilisha Mwanasheria Mkuu wa Serikali Anjelina Chacha, alimuomba Jaji huyo mahakama kutoa taratibu wa watu kuingia mahakamani hapo kwa wale wanaokosa nafasi za kukaa, wasiingie mahakamani na kusimama.
Kimomogolo alikubaliana na wenzake na kudai kuwa kutokana na mazingira ya mahakama kesi hiyo haiwezi kuendelea ambapo alimuomba Jaji kuahisisha kesi hiyo hadi leo.
Aidha Kimomogolo aliikumbusha mahakama hiyo amri iliyotolewa na Jaji
huyo kwa Msajili wa Wilaya kuhakikisha vipaza sauti vinawekwa ili watu
waliopo nje ya mahakama waweze kusikia kianchoendelea ndani ya
mahakama hiyo. Awali kesi hiyo ilikwama kusikilizwa Jumatatu hii baada ya Jaji anayesikiliza shauri hilo Mujulizi kupata dharura ya (safari).
Mujulizi ameahirisha shauri hilo hadi leo na kusema kuwa kesi hiyo
itaanza kusikilizwa kwa utaratibu utakaowekwa na mahakama hiyo, ikiwemo kiasi cha watu watakaoingia.