Tupambane na uharibifu wa mazingira- Dk Shein

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Ali Mohamed Shein

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, amesema ipo haja ya kushirikiana katika kupambana na uharibifu wa mazingira kutokana na athari zake kujitokeza kwa wingi. Nchi ya Finland kwa kuiunga mkono Zanzibar katika juhudi za uhifadhi wa mazingira.

Dk. Shein alieleza athari za uharibifu wa mazingira na kusisitiza kwamba unachangia sana kuleta mabadiliko ya tabia nchi kwa pamoja zimeaanza kuleta athari katika visiwa vya Zanzibar na kusisitiza haja ya mashirikiano ya pamoja katika kupiga vita uharibifu wa mazingira.

Dk. Shein aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Waziri anayeshughulikia Maendeleo ya Kimataifa kutoka Finland, Bi Heidi Hautala, Ikulu mjini Zanzibar. Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alitoa shukurani kwa Finland kutokana na uungaji wake mkono mkubwa kwa Zanzibar katika suala zima la uhifadhi wa mazingira, ardhi, misitu na masuala mengine ya kimaendeleo.

Dk. Shein alieleza kuwa athari juu ya mazingira zimeanza kujitokea sehemu mbali mbali za visiwa vya Unguja na Pemba na kutolea mfano athari zilizoanza kujitokeza katika kisiwa Panza huko Pemba pamoja na maeneo ya Kaskazini mwa Unguja na maeneo mengineyo zikiwemo fukwe.

Aidha, Dk. Shein alieleza uharibifu wa mazingira unaotokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuni, makaa, ujenzi, uchimbaji mchanga na mawe na mambo mengineyo ambayo ndio chanzo kikuu cha athari za mazingira nchini.

Alieleza kuwa mbali ya maeneo mengi yaliokubwa na athari hizo kwa hapa Zanzibar pia, kuna maeneo mbali mbali nayo yameanza kuathirika huko Tanzania Bara. Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na athari hizo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikichukua jitihada za makusudi katika kuhakikisha miti zaidi inapandwa kwa lengo la kuhifadhi mazingira sanjari na uendelezaji wa program ya hifadhi ya mazingira inayoendeshwa na mradi wa SMOLE.

Akieleza juu ya uhusiano kati ya Zanzibar na Finland, Dk. Shein alisema kuwa nchi mbli hizo zina uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu. Kwa upande wa Utawala Bora, Dk. Shein alisema kuwa Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo katika bara la Afrika kuusimamia kikamilifu Utawala Bora kwa kuazisha Wizara inayohusiana na sekta hiyo.

Dk. Shein alisisitiza kuwa Tanzania imeweza kujijengea mlahaka mzuri Kitaifa, hatua ambayo imepelekea kujenga uhusiano na ushirikiano mwema na kueleza kuwa Finland kusaidia kuanzishwa kwa Taasisi ya Uongozi huko Dar-es-Salaam kutaisaidia hata Zanzibar.

Nae Waziri anayeshughulikia Mandeleo ya Kimataifa wa Finland Mhe. Heidi Hautala alimuhakikishia Dk. Shein kuwa Finland itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kuahidi kuisimamia vyema miradi inayoidhamini.

Waziri Hautala alisema kuwa Finland inathamini uhusiano na ushirikiano mkubwa uliopo kati ya Zanzibar na Tanzania kwa jumla pamoja na nchi zote zilizopo Mashariki mwa Afrika.

Waziri huyo aliahidi kuendelea kuiimarisha miradi inayofadhiliwa na nchi hiyo ikiwa ni pamoja na miradi ya uhifadhi wa mazingira na misitu. Kwa upande wa Ushirikiano wa Kimataifa Waziri Hautala alieleza kuwa Finland itaendelea kuimarisha uhusiano uliopo kati yake na Tanzania ikiwemo Zanzibar.

Viongozi walieleza haja ya uimarishaji wa sekta ya utalii hapa nchini ambapo Dk. Shein alimueleza Waziri huyo juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kuiimarisha sekta hiyo ambayo imekuwa ikichangia pato la taifa.

Nae Balozi wa Finland nchini Tanzania Sinikka Antila ambaye aliongozana na Waziri huyo, alimueleza Dk. Shein kuwa tayari wameshakubaliana na Wizara husika kupitia Mradi wa SMOLE kuanzisha tovuti maalum itakayoonesha masuala ya mazingira ya Zanzibar zikiwemo ramani.