HakiElimu yakabidhi maktaba shuleni Mwisenge

Nembo ya taasisi ya Hakielimu

Na Joachim Mushi

TAASISI ya HakiElimu leo inakabidhi jengo la maktaba katika Shule ya Msingi Mwisenge ikiwa ni heshima ya kumuenzi Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere kwa moyo wake wa kupenda kujisomea vitabu mbalimbali.

Akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari leo, Mkurugenzi Mtendaji wa HakiElimu, Elizabeth Missokia amesema taasisi yake imekabidhi maktaba hiyo ikiwa ni maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru, na kuufanya umma ujenge utamaduni wa kuipenda elimu kama alivyofanya Nyerere enzi za uhai wake.

“Tumeijenga maktaba hii kwa heshima aliyonayo Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ambaye alisoma Shule hii mwaka 1934 hadi 1936. Wakati Taifa linaadhimisha mia 50 ya Uhuru tumeona ni kitendo cha kiungwana kutambua msingi aliyotuachia wa kusoma vitabu,” alisema Missokia katika taarifa yake.

Alisema enzi za uhai wa Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere alipenda elimu hivyo taasisi hiyo imeona njia pekee ya kumuenzi ni kujenga maktaba katika shule ambayo alisoma. Amesema pamoja na mambo mengine maktaba hiyo imejengwa ili kuamsha ari ya kusoma kwa wanafunzi, walimu na jamii inayoizunguka Shule ya Mwisenge.

Alisema HakiElimu inaamini maktaba ni sehemu muhimu katika kuboresha taaluma katika shule ama taasisi ya elimu na pia ni sehemu muhimu kwenye mchakato wa kujifunza.

“Mwalimu huwapatia wanafunzi sehemu tu ya maarifa darasani, lakini mwanafunzi anapaswa kuongeza maarifa zaidi kwa kusoma vitabu. Kwa mfano Mwalimu Nyerere alipenda sana kusoma na katika uhai wake alisisitiza umuhimu wa kusoma,” alisema Missokia.

Aidha alisema ujenzi wa maktaba hiyo iliyogharimu sh. Milioni 42, ikiwa na vitabu na thamani zake, kunakamilisha jumla ya maktaba za jamii 32 ambazo zimejengwa na HakiElimu nchi zima hadi sasa.