Jenerali Mboma ateuliwa M/Kiti Bodi ya Tanesco

Jenerali mstaafu wa JWTZ, Robert Mboma

Na Mwandishi Wetu

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Kikwete amemteua Jenerali mstaafu Robert Mboma kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo jijini Dar es Salaam na Ofisa Mawasiliano wa Wizara ya Nishati na Madini, Greyson Mwase inasema uteuzi huo unaanzia Oktoba 27, 2011 baada ya Bodi iliyokuwepo kumaliza muda wake yaani Oktoba 26, 2011.

Aidha amesema sambamba na uteuzi huo Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja kwa mamlaka aliyonayo naye amewateua wakurugenzi wanane wa Bodi ya Wakurugenzi ya Shirika la Umeme Tanzania Oktoba 27, 2011.

Taarifa hiyo imesema wajumbe walioteuliwa ni pamoja na Baruany Elijah Luhanga, Ridhiwan Ali Masudi, Leonard R. Masanja, Vintan W. Mbiro, Beatus P. Segeja, Hassan Ally Mbaruk, Victor K. Mwambalaswa (Mb.) na Abdul Ibrahim Kitula.

Sheria ya Mashirika ya Umma Sura 257 kama ilivyorekebishwa mwaka 2002 (The Public Corporations Act, Cap. 257 of R.E. 2002), inampa mamlaka rais wa nchi kumteua Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TANESCO, huku waziri akiteua wajumbe wa bodi hiyo.