TANZANIA itapata heshima kubwa iwapo Jaji Mkuu Mheshimiwa Mohammed Chande Othman atachaguliwa kuwa muongoza Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai, maarufu kama International Criminal Court (ICC), yenye makao yake makuu mjini Haque, Nertherlands baada ya kumalizika kwa muda wa Jaji Jose Luis Moreno Ocampo anayemaliza muda wake.
Jina la Jaji Othman ni moja kati ya majina manne yaliyopendekezwa na Kamati Maalum inayoundwa na mabalozi. Nafasi hii huwa haiombwi bali Kamati Maalum hukaa na kupendekeza majina ambayo hupitia mchujo ndani ya kamati hiyo na hatimaye kupata jina moja.
Wengine waliopendekezwa ni kutoka Gambia, Uingereza na Uhispania.
Kama Jaji Mkuu atapata nafasi hii, atakuwa ametumikia serikali kwa muda mfupi sana baada ya kuteuliwa na Rais Jakaya Mrisho Kikwete kushika wadhifa huo serikalini.
Hata hivyo, Rais anaona jambo hili ni jema, si kwa Mheshimiwa Chande tu, bali hata kwa nchi ya Tanzania, na anaona hili ni jambo jema na ambalo litailetea sifa nyingi na kuiweka Tanzania katika ramani ya mambo makubwa na muhimu yenye dhamana kubwa ulimwenguni.
Rais anamtakia Jaji Othman Heri na akifanikiwa kupata nafasi hiyo, Rais atakubaliana na uteuzi huo na itambidi ateue Jaji Mkuu mwingine kutokana na majaji wengi tulio nao Tanzania.
Jaji Mkuu Othman ameshika wadhifa wa Jaji Mkuu wa Tanzania kuanzia tarehe 28 Disemba, 2010 baada ya kustaafu kwa mujibu wa sheria kwa Jaji Augustino Ramadhani aliyestaafu tarehe 27 Disemba, 2010.
Jaji Othman amekuwa Jaji wa Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa kwa muda wa miaka saba, amekuwa mtaalamu binafsi juu ya hali ya Haki za Binadamu huko Sudan Kusini hadi mwezi August, 2011.
Jaji Othman amezaliwa tarehe 1Januari, 1952, ana shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo Kikuu cha Dar-Es-Salaam na Shahada ya Uzamili kutoka Chuo Kikuu cha Webster, Geneva-Uswis.
Pia amewahi kuwa Mwendesha Mashtaka wa Mahakama ya Rwanda huko Arusha na pia kawahi kushika nafasi sawa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali huko Timor Mashariki.